KIJANA Frank Mboma (19) aliyedaiwa kufa katika mji wa Mbalizi kwa kupigwa na wananchi wenye hasira na kuzikwa eneo hilo juzi alizua tafrani baada ya kuibuka msibani akitokea Tunduma.
Sakataka hilo lilitokea Jumatano wiki hii katika kijiji cha DDC mji mdogo wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya Vijijini baada ya kijana huyo kufika nyumbani kwao na kukuta watu wameweka tanga.
Kitendo hicho kilizua tafrani na waombolezaji hao kutimua mbio wakidhani muzimu umeibuka.
Majira baada ya kusikia taarifa hizo, lilifuatilia hadi kijijini hapo, umbali wa kilomita 15 kutoka Mbeya mjini kujionea kulikoni.
Akithibitisha kutokea tukio hilo Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bw. Joines Mwalusanya, alisema kifo hicho kilitokea June 27 mwaka.
Alisema walipelekewa taarifa ofisi ya kijiji kuwa kuna kijana amepigwa na wananchi wenye hasira na amefia Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Alisema waliambatana na ndugu wa kijana huyo kwenda kutambua maiti Hospitali ya Rufaa Mbeya na kubaini kuwa marehemu huyo alikuwa ni Frank.
Hata hivyo, alisema babu wa kijana huyo Mzee Joyasi Mboma alikataa kuwa kijana huyo si mjukuu wake Frank kutokana na kuonesha tofauti za sehemu fulani mwilini japo alionekana kufanana naye kwa sehemu kubwa.
Baadaye alisema bibi wa kijana huyo na kinyozi aliyekuwa amemnyoa, walithibitisha kuwa ndiye na kuamua kuchukua kibali Polisi na kuzika Juni 29 jioni na kuendelea na matanga nyumbani kwa Mzee Mboma eneo hilo la DDC.
Naye Mzee Mboma ambaye amemlea kijana huyo akitoa maelezo yake kwa waandishi wa habari alisema mjukuu wake aliondoka wiki moja kwenda Tunduma kutafuta maisha hadi aliposikia habari kwamba kuna maiti inayofanana naye na baada ya utata alikubali kuzika mwili huo.
Alisema kuwa alishangaa Jumatano kufuatwa na watu na kuambiwa mjukuu wake amefika eneo jirani na kwake na anaogopa kuingia ndani baada ya kuambiwa alikuwa amekufa na kuzikwa na watu wamekusanyika kwa ajili ya msiba wake.
"Nilikwenda ingawa ilikuwa usiku wa manane, nilishangaa kumkuta Frank akiwa hai. Nilimchukua na kuingia naye ndani, baada
ya kumhoji tuligundua kuwa ni mjukuu wangu na tuliyemzika siye,"alisema Mzee Mboma.
Alisema kuwa kesho yake walikwenda Polisi kutoa taarifa na kuambia waende na Frank kwa ajili ya mahojiano zaidi ili kuondoa utata.
Akiwa Polisi Frank alieleza kuwa baada ya kwenda Tunduma kutafuta maisha alijisikia roho ikiuma na kuamua kurudi kwao mara moja ndipo alipokuta msiba wake bandia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Bw.Advocate Nyombi hakupatikana kuzungumzia sakata hilo lakini ofisa mmoja katika ofisi yake ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa kuwa si msemaji, alisema wamepata taarifa za tukio hilo na walikuwa wanasubiri maelezo kamili kutoka kwa maafisa wa Jeshi hilo waliokuwa wakifuatilia tukio hilo.
Categories: