Idadi ya wanafunzi waliofaulu kuingia kidatu cha tatu kwa mwaka 2010 imeongezeka kwa asilimia 58.2 kutoka asilimia 54.2 ya mwaka 2009, huku skuli ya Kajengwa wilaya ya kusini ikishika nafasi ya kwanza.
Taarifa ya matokeo ya mtihani wa darasa la saba na kidato cha pili ya mwaka 2010 iliyotolewa na wizara ya elimu imesema jumla ya wanafunzi elfu 19, 855 waliofanya mtihani kati yao elfu 11, 562 wamefaulu kuingia kidatu cha tatu.
Taarifa hiyo imesema jumla ya wanafunzi elfu moja 610, wakiwemo wanawake elfu moja na 49 hawakufanya mitihani kwa sababu mbali mbali, huku kukiwa na kesi 58 za udanganyifu.
Skuli tatu bora zilizofanya vizuri ya kwanza ni skuli ya sekondari ya Kajengwa wilaya ya Kusini, skuli ya Kiuyu wilaya ya Micheweni na skuli ya Maungani wilaya ya magharibi.
Skuli zilizofanya vibaya ni Mwambe Shamiani ambayo haikupasisha mwanafunzi hata mmoja, skuli ya Mgogoni wanafunzi wanane, skuli ya Umbuji wanafunzi sita, skuli ya Michamvi wanafunzi saba na skuli ya Shengejuu mwanafunzi mmoja ambapo kwa sasa skuli hizo hazitakuwa na madarasa ya kidatu cha tatu.
Kwa upande wa darasa la Saba jumla ya wanfunzi elfu 18, 908 wamechaguliwa kuingia kidatu cha kwanza sawa na asilimia 81.2 kati yao wanafunzi mia moja na 77 wataingia madarasa ya vipawa maalum na 952 wamechaguliwa kuingia mchipuo.
Skuli bora kwa upande wa darasa la Saba ya kwanza ni Kizimbani Pemba, Mtiulaya na Jongowe Unguja na skuli zilizofanya vibaya Kandwi, Mkokotoni na Kikobweni zote za Unguja. Majina ya wanafunzi hao yanatarajiwa kutangazwa leo.