MABAO ya Samuel Eto'o,dakika ya 10 ya kipindi cha kwanza na Lionel Messi, dakika ya 70 yameipa ubingwa wa tatu wa Ulaya Barcelona na kuivua ubingwa huo Manchester United.
Mpira wa kwanza wa Barca, uliomaliza utawala wa dakika 10 za kwanza za mchezo huo lilifungua mlango kwa mabingwa hao wa Hispania kuonyesha dhamira ya ushindi.
Eto'o, alibashiriwa mapema na mkongwe Rui Costa wa Ureno kuwa ndiye angeweza kuipatia timu yake bao la dakika za nyongeza na kuwaduwaza Man United.
Mshambuliaji huyo wa Cameroon aliweza kutimiza ubashiri huo, kwa kuipa Barca bao muhimu ambalo hatimaye lilireejeshea jeuri timu yake na kuanza kutawala sehemu kubwa ya mchezo kipindi cha kwanza.
Mchezo ulianza kwa timu hizo kuonyesha makali, ingawa ilikuwa Man United ambayo ilikuwa na uchu kwa kulishambulia lango la Barca na kupata mikwaju kadhaa ya adhabu ndogo ambayo 'mtaalam' wake, Cristiano Ronaldo alishindwa kuitumia.
Katika mchezo huo, mwamuzi Massimo Busacca, ambaye kabla ya mchezo alikwenda Vatican, makao ya Kanisa Katoliki, kuomba baraka kwa Papa Benedict XVI akimwonyesha kadi ya njano Gerrard Pique kwa kumchezea vibaya Ronaldo.
Nao Ronaldo na Paul Scholes walionyeshwa kadi za njano kwa mchezo mbaya dhidi ya wapinzani wao.
Mabadiliko ya kipindi cha pili ya kocha Alex Ferguson kuwatoa Ji- Sung Park na Anderson na kuwaingiza Carlos Tevez na Scholes hayakusaidia.
Vikosi:
Barcelona - Victor Valdes, Carles Puyol, Gerrard Pique, YayaToure, Sylvinho, Xavi Hernandez , Sergio Busquets, Andres Iniesta, Lionel Messi, Samuel Eto'o, Thierry Henry.
Manchester United: Edwin Van der Sar, John O'Shea, Rio Ferdinand, Nemanja Vidic, Patrice Evra; Anderson, Michael Carrick, Ryan Giggs, Ji- Sung Park, Cristiano Ronaldo, Wayne Rooney.