Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Wabunge waondolewa ulaji

-
Rehema Mwinyi.

Wabunge wameanza kunyang’anywa sehemu ya ulaji kutokana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoa waraka unaowaelekeza wabunge wote ambao ni wajumbe kwenye bodi za mashirika na taasisi za fedha kuondolewa mara moja. Hatua hiyo inatokana na ushauri uliotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kushauri wabunge wasiwe wajumbe wa mashirika yoyote ya umma, ili kuondoa mgongano wa maslahi. Kaimu Msajili wa Hazina, Godfrey Sella, alisema jana kuwa utekelezaji wa waraka huo wa BoT unaanza mara moja. Alisema kuna baadhi ya wabunge wenye maslahi katika taasisi za kifedha; hivyo si vizuri viongozi hao kuwa sehemu ya bodi za wakurugenzi.

Tayari BoT imetoa orodha ya wabunge wote ambao ni wajumbe kwenye taasisi za fedha na imepeleka waraka huo kwa Msajili wa Hazina ili aondoe majina ya wabunge hao kwenye bodi hizo. “Lengo hapa ni kutenganisha usimamizi na utekelezaji…tumepata waraka huo wa BoT na kinachofuata ni utekelezaji,” alisema Sella wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Tandahimba, Juma Njwayo (CCM), aliyehoji sababu ya wabunge wapigwe marufuku kuwa wajumbe wa mashirika ya umma wakati kuna baadhi yao wana uwezo.

Mbunge huyo alisema kama kuna chama cha siasa kimeshinikiza suala hilo ni vyema kikapuuzwa; kwa kile alichodai kuwa kufanya hivyo ni kutowatendea haki wabunge, kwani nao ni sehemu ya jamii. “Kuna wabunge wana uwezo mkubwa wa kuisaidia Serikali kupitia mashirika haya, iweje waondolewe kwenye nafasi zao za ujumbe wa bodi za mashirika ya umma?” alihoji mbunge huyo. Baada ya swali hilo, Mwenyekiti wa PAC, Kabwe Zitto, alifafanua kuwa hakuna chama cha siasa ambacho kimekuwa kinashinikiza suala hilo; ila ni ushauri uliotolewa na ofisi ya CAG.

Ndipo Kaimu Msajili wa Hazina akafafanua, kwamba tayari hatua zimeanza kuchukuliwa na akaeleza kuwa zina nia nzuri ya kuwafanya wabunge wawe wasimamizi wazuri wa mashirika hayo. Wakati huo huo, Msajili huyo wa Hazina alikiri kuwa kampuni za Meremeta na Buhemba hazijawasilisha hesabu zozote katika ofisi yake kwa kile alichodai kuwa wizara ndiyo yenye jukumu la kuomba hesabu hizo. Alisema Meremeta ambayo iko chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, haina hesabu zozote lakini pia BoT ambayo inahusika na kampuni hiyo nayo haina hesabu zake.

“Hii inahesabika kama ni kitegauchumi cha serikali, lakini kwa mtazamo wangu, si shirika la kitega uchumi kwani hata CAG ameshindwa kuifanyia ukaguzi, kwa vile haina mali inayoonekana kwa macho,” alisema Sella. Kuhusu majukumu ya ofisi ya Msajili wa Hazina, Kaimu Msajili huyo alilalamika kuwa ofisi yake imejikuta wakati mwingine ikifanya kazi za ndani za mashirika ya umma kutokana na mfumo wa kiutendaji uliopo. Alisema kwa sasa wanajitahidi kuandaa waraka utakaosaidia kufanya mabadiliko ili ofisi ya Msajili wa Hazina ibaki kuwa msimamizi wa mashirika ya umma bila kuingilia utendaji wa mashirika hayo.

“Tunataka sisi tubaki kusimamia na kuona kama uamuzi unaofanywa na mashirika haya unazingatia maslahi ya taifa,” alisema. Hata hivyo alisema kwa sasa wizara nyingi ambazo zinatakiwa zipeleke mapendekezo ya wajumbe wa bodi wa mashirika mbalimbali kabla ya kutangazwa, hazifanyi hivyo. Alisema licha ya sheria kuzitaka kufanya hivyo kwa makusudi, mawaziri wanakaidi. “Ukihoji utaulizwa Msajili ni nani na ukisema ufuate sheria lazima utagongana na wakubwa zako, ndiyo maana tunaamua kukaa kimya.”



Leave a Reply