Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Kikwete ashutumiwa vikali kwa kuendekeza ziara za nchi za nje

-
Rehema Mwinyi.




WAKATI Rais Jakaya Kikwete akirejea nchini kutoka Marekani kwa ziara ya siku takriban nane, jarida maarufu la uchambuzi wa kiuchumi, The Economist limehoji safari za mkuu huyo wa nchi, likisema kuwa anatumia muda mwingi katika kutangaza jina la nchi nje badala ya kutatua matatizo ya ndani.

Kikwete, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kabla ya kuingia Ikulu, ameshakwenda Marekani zaidi ya mara sita tangu ashike serikali ya awamu ya nne, ikiwa ni baadhi ya safari zake nje ya nchi alizofanya katika kipindi cha miaka mitatu na nusu hadi sasa.

Safari hizo zimewafanya watu mbalimbali, wakiwemo wanasiasa na wachumi kuhoji sababu za safari hizo, ambazo wakati fulani aliwahi kuzitetea kuwa zina tija katika kuitangaza nchi na kuvutia wawekezaji.

Katika habari ya uchambuzi wa toleo la Mei 7, gazeti la The Economist limeeleza jinsi Tanzania inavyohaha kusaka misaada nje ili kukabiliana na kuyumba kwa uchumi duniani wakati bajeti yake inafadhiliwa kwa asilimia 40.

"Ni kiasi gani kinatosha," inahoji habari hiyo ya uchambuzi yenye kichwa cha habari kisemacho, "Tanzania: Waiting for That Great Leap Forward (Tanzania: Ikisubiri Kupiga Hatua Kubwa Mbele)."

Habari hiyo inasema: "Nchi tayari inapata asilimia 40 ya bajeti yake ya serikali kutokana na misaada, lakini inataka fedha zaidi ili iweze kukabiliana na kuporomoka kwa uchumi. Ni kiasi gani kinatosha?"

Baadaye gazeti hilo linaloheshimika kwa uchambuzi wa mambo ya kiuchumi duniani, linamkariri Rais Kikwete akizungumza katika moja ya hotuba zake kwa kusema: "Tunajaribu kupunguza utegemezi wetu, lakini tunashukuru kwa kila tunachokipata."

Bajeti ya mwaka huu ya serikali ilikuwa Sh7.22 trilioni huku asilimia 33.6 ikiwa ni fedha kutoka kwa wahisani na mwaka ujao wa fedha bajeti ya serikali inatazamiwa kuwa Sh8.14 trilioni, huku kiasi cha fedha kutoka kwa wahisani kikitegemewa kupanda kutoka asilimia 33.6 hadi asilimia 34.3.

Mwaka jana, wahisani hawakutoa karibu dola 2.4 bilioni za Marekani walizoahidi na hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika mwaka mpya wa fedha kutokana na nchi wahisani kulazimika kutoa fedha kuokoa taasisi zao za kifedha zilizoathiriwa na mtikisiko wa kifedha duniani ulioyumbisha uchumi wa dunia.

Katika uchambuzi wake, linasema Tanzania, ikiwa na idadi ya watu milioni 44, ina utulivu kulinganisha na nchi jirani ya Kenya, yenye watu milioni 40.

"Inachokosa kiuwezo ndicho kinasaidia kuwa na utulivu na utambulisho wa utaifa. (Nchi) haiwezi kusambaratika wakati wa uchaguzi au wakati wowote ule," linaandika gazeti hilo.

Linasema chama kilichopigania uhuru, CCM, ambacho zamani kilijulikana kama Tanu, bado kinahangaishwa na vyama hohehahe vya upinzani.

"Bwana Kikwete ni mtu wa CCM; kazi aliyoibukia ni ya kiongozi wa vijana aliyehusika na kutangaza siasa kwenye jeshi. Ni wazi kuwa atarejea madarakani kwa ushindi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu ujao. Bado anashawishi wawekezaji kwa kutumia kipaji chake kama mtu wa (idara ya) masoko," linaandika The Economist.

"Lakini bado wale walioanzisha maduka nchini kila mara wanakerwa. Wengi wanalalamika kuwa Tanzania ni goigoi au hata kueleza kuwa ni sehemu mbaya kufanya biashara na haina shukrani kwa misaada (inayopata) au uwekezaji.

"Hata wanaoitetea wanakiri kuwa imegubikwa na urasimu na haina wafanyakazi walio na stadi. Karibu kila mtu anasema Kikwete anatumia muda mwingi mno kutangaza nchi nje na si kutatua matatizo ya nyumbani kwa kiasi cha kutosha. Mwaka jana alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika."

Hata hivyo, gazeti hilo la Marekani linasifu kipaji cha Kikwete katika kushawishi; na imani kubwa aliyonayo kwa maendeleo, likisema kuwa ana imani kuwa misaada itaifanya Tanzania iendelee kuwa juu kiuchumi kwa muda mrefu na hatimaye kupiga hatua kubwa kwenda mbele.

"Maghorofa mapya yanayong'aa, yaliyo hata kwenye miji midogo, sambamba na barabara na miradi mipya ya maji inadhihirisha imani hiyo (ya Kikwete). Hali ya siasa ni imara. Wapinga Muungano kwenye visiwa vya Zanzibar wametulia kwa sasa," linaeleza gazeti hilo.

Gazeti hilo pia linaeleza hali ya uharaka iliyopo sasa kwenye serikali ya Rais Kikwete, likitoa mfano wa waziri anayehusika na nishati kuwa anataka kituo kipya cha umeme katika muda mfupi ili kukabiliana na kuanguka kwa huduma ya nishati hiyo, huku JK akiita viongozi wa mashirika yanayomilikiwa na serikali kama Mamlaka ya Bandari na Kampuni ya Reli akitaka ufanisi.

Bila kufafanua zaidi, pia limeandika kuwa, Rais Kikwete anawashughulikia watu wanaoitwa "Wabenzi", likidai kuwa ni wale wanaoendesha magari ya kifahari kama ya Mercedes Benz.

Lakini linadai kuwa, Tanzania kwa kiasi fulani, imeshindwa kwenda na wakati au haikupata mafanikio.

"Ziara ya rais wa China ya hivi karibuni imeshindwa kutoa uwekezaji mwingi," linaeleza gazeti hilo. "Serikali ya China inadhani Kenya, na si Tanzania, ndio njia ya kupitia kwenda kwenye utajiri wa madini wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

"Reli mbili za Tanzania (reli ya kati na Tazara) ni mikweche. Bandari ya Dar es Salaam ilishindwa kupoka biashara kutoka Bandari ya Mombasa wakati Kenya ikiwa kwenye vurugu mwaka mmoja uliopita.

"Hakuna mtu anayeonekana kujua ni lini bandari hiyo kubwa itafikia malengo yake ya kupunguza mrundikano wa mizigo bandarini ifikapo mwaka 2030."


Leave a Reply