Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

JK kuongoza mkutano wa kujadili kilimo

-
Rehema Mwinyi.

Rais Jakaya Kikwete wiki ijayo ataongoza mkutano wa kujadili kilimo kuwa nguzo kuu ya uchumi wa Tanzania. Mkutano huo wa siku mbili ulioandaliwa na Baraza la Biashara la Taifa (TNBC), pia utahudhuriwa na Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, mawaziri, wakuu wa mikoa, wajumbe wa baraza hilo, wawekezaji wa ndani, wadau wa maendeleo, wasambazaji wa mazao na wasindikaji. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dunstan Mrutu alisema mkutano huo utajulikana kwa jina la 'Kilimo Kwanza ' ukiwa na nia ya kufanya tathmini kwa nini sekta ya kilimo imeshindwa kukua na kupunguza umasikini.

Mrutu alisema mkutano huo utafanyika Juni 2 hadi 3 mwaka huu Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza hilo. Alisema lengo la ‘Kilimo Kwanza’ ni kuwezesha Mapinduzi ya Kijani kwa kuwa na kilimo cha teknolojia ya kisasa hasa katika kilimo na ufugaji, kutumia mbegu bora na za kisasa, uzalishaji kwa chupa, dawa za kilimo, mbolea na kukuza kilimo cha umwagiliaji. “Mkutano huu utakaowashirikisha wakuu wa nchi na mikoa, utasaidia kuangalia matatizo mbalimbali yanayosababisha kilimo kushindwa kukua na jinsi ya kufanya ili kukuza sekta hiyo,” alisema Mrutu.

Alisema mkutano huo utasaidia kubadilisha kilimo cha Tanzania kuwa cha kisasa na kibiashara kwa kuwashirikisha wakulima wadogo na wakulima wakubwa kuachana na jembe la mkono na kutumia zana za kisasa na kuacha kuuza mazao yasiyosindikwa. Alisema baada ya mkutano huo, uamuzi utakaofikiwa utasimamiwa na wakuu wa mikoa washiriki wa mkutano huo ili kuhakikisha kilimo kinakua na kuinua uchumi na kuacha kutegemea vitu kutoka nje.

Leave a Reply