Uchanguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Busanda, wilayani Geita, mkoani Mwanza, unafanyika leo baada ya hekaheka za kampeni za takribani siku 20 huku Tume ya Uchaguzi (NEC) ikiviasa vyama vinavyohusika kuheshimu kanuni na sheria kwa kuepuka vurugu. Mwenyekiti wa Tume, Jaji Lewis Makame, jana alisema kwamba NEC ilipata taarifa juu ya kuwapo mchezo mchafu wakati wa kampeni na alivitaka vyama vya siasa kutowashawishi wafuasi wao kwenda kinyume na taratibu na kusababisha vurugu katika uchaguzi wa leo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Jaji Makame alisema, “tume imekuwa ikifuatilia kwa karibu sana wakati wote wa kampeni za uchaguzi na haikufurahishwa na matukio machache ya kuvuruga mchakato wa uchaguzi jimboni Busanda ambayo yameripotiwa katika vyombo vya habari.” Kwa mujibu wa Jaji Makame, matukio hayo ni pamoja na kutukanana, kukashifiana, mapigano, ununuzi wa shahada na utoaji wa chumvi kwa wapiga kura ambao aliutaja kwamba ni rushwa. Jaji Makame aliwataka wapiga kura kuhakikisha kwamba kila atakayeingia katika kituo cha kupigia kura anapewa karatasi iliyopigwa muhuri wa kituo nyuma yake na isiwe na alama zozote zisizohusika.
Wakati huo huo wiki hii HabariLeo Jumapili ilifuatilia habari zilizochapishwa katika magazeti yaliyo na waandishi katika kampeni hizo za Busanda na kubaini mgawanyiko mkubwa wa vyombo hivyo katika misingi ya vyama. Tathimini ya habari hizo ilionyesha kuwa vyombo hivyo vya habari viliripoti zaidi habari za kampeni za Chadema na CCM huku CUF na UDP ‘vikisuswa’ na kuonekana kama havipo katika kampeni hiyo.
Pia ilibainika kuwa viongozi wa kitaifa wa vyama hivyo vya Chadema na CCM na matukio yaliyohusu vyama hivyo viwili, yalipamba vichwa vya habari vya kurasa za mbele na picha na kuwafunika wagombea ambao ndio watakaopigiwa kura na leo na kutakiwa kuwajibika kwa wananchi. Kwa mujibu wa tathmini hiyo, licha ya habari za CCM na Chadema kuwa habari kubwa zilizotawala wiki hii, wagombea katika habari hizo walizibwa midomo kwa kutajwa majina bila kuwapo habari zao na pale walipopewa nafasi, walipewa aya zisizozidi mbili katika habari ambazo zingine zilifikia ukubwa wa aya zaidi ya 15.
Mmoja wa maofisa wa kitaifa wa CUF, Mbarara Maharagande, alipozungumza na HabariLeo Jumapili kuhusu mwenendo huo wa vyombo vya habari alisema chama hicho kimeliona na baada ya uchaguzi kitatoa tamko. Naye Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo ambaye alikuwa Afrika Kusini, alisema kampeni za chama hicho hazikuonekana kuwa habari kwa kuwa hazikuwa na matusi na vurugu.
“Ni bahati mbaya sana tumerithi vyombo vya habari vya aina hii, tukielezea sera na amani si habari lakini matusi na vurugu kwao ndio habari,” alisema Cheyo. Katika uchaguzi huo ambao idadi ya wapiga kura waliojiandikisha ni 135, 168 na vituo vya kupigia kura ni 380, Msimamizi wa Uchaguzi, Dani Mollel alisema kuwa wamejiandaa vyema kuhakikisha kwamba unakwenda kama ulivyopangwa. Gazeti hili lilishuhudia magari yaliyokuwa yakipakia vifaa mbalimbali kutoka ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita, kwa ajili ya kuvisambaza kwenda katika maeneo ya uchaguzi.
Hata hivyo mwenendo wa kampeni unaonyesha kuwa wakati vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo ni vinne, lakini CCM na Chadema ndivyo ambavyo vimekuwa vikiteka mijadala ya kisiasa na kuonyesha mwelekeo kwamba kimojawapo kitaibuka mshindi. Akizungumza na gazeti hili, mgombea wa CCM, Lolesia Bukwimba (38) alisema ana uhakika wa ushindi na kwamba atahakikisha anaendeleza shughuli mbalimbali za maendeleo kama alivyoahidi kwa kuzingatia ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2005. Hata hivyo, alikiri kwamba katika uchaguzi lolote laweza kutokea na akasema yuko tayari kupokea matokeo yoyote.
Alisema ikitokea akashindwa, ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida na kujishughulisha na shughuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukijenga chama katika jimbo hilo. Naye mgombea wa CUF, Oscar Ndalahwa (52) alisema yuko tayari kwa matokeo yoyote ikizingatiwa kwamba yeye ni mwanamichezo anayeamini kwamba katika ushindani wowote lazima pawepo mshindi na atakayeshindwa. Kwa mujibu wa Ndalahwa, yeye ni Mwenyekiti wa Timu ya Mpira wa miguu wa Kijiji cha Nyarugusu ambayo imeifikisha timu hiyo katika Ligi Daraja la III ngazi ya mkoa.
Kwa upande wa Chama cha United Democratic (UDP), mgombea wake, Beatrice Lubambe ambaye ni mfanyabiashara, pia alisema yuko tayari kukubaliana na matokeo iwapo hapatakuwapo aina yoyote ya mizengwe katika uchaguzi. Ingawa gazeti hili halikumpata mgombea wa Chadema, Finias Magesa (52) kuzungumza naye moja kwa moja kuhusu msimamo wake, lakini kupitia majukwaa ya mikutano ya hadhara, alisema anajiamini na atakapochaguliwa atahakikisha kwamba anatumia fedha zake kuleta maendeleo ikiwemo kusomesha yatima.
Kuhusu mjadala juu ya nani atashinda katika uchaguzi huo, Chadema kimekuwa kikitajwa kutokana na vigezo vya namna ambavyo chama hicho kimekuwa kikiendesha kampeni zake na kuvuta hadhara hususan ya vijana na wakazi wa maeneo ya mjini. Ujio wa helikopta sambamba na ushawishi wa majukwaani na hata nje ya majukwaa unaofanywa na Chadema chenye vijana wengi, ni miongoni mwa hoja ambazo zinatumiwa kubashiri kwamba mgombea wake, Magesa atashinda.
Ingawa kumekuwapo na madai kwamba Chadema kinashabikiwa zaidi mijini na kwamba mashabiki wake wengi siyo wapiga kura, lakini Ofisa Habari wa chama hicho, David Kafulila aliliambia gazeti hili kwamba kimejiweka sawa hadi ngazi ya kituo “Sisi tunaongoza kwa kufanya kampeni ya kisayansi. CCM wao wanajivunia viongozi wa ngazi ya kijiji. Chadema tuna timu hadi ngazi ya kituo; tunafahamu ni nani atampigia Chadema na ni nani atampigia CCM,” alisema Kafulila na kusema tathmini waliyofanya, inaonyesha watashinda kwa asilimia 78. Kwa upande wa CCM ambacho mgombea wake ni Lolesia Bukwimba, kimekuwa kikitajwa na mashabiki wake kwamba kitashinda kutokana na madai kwamba kina wafuasi wengi vijijini ambao asilimia kubwa ni wapiga kura.
Wachambuzi wengine wanaoiunga mkono CCM, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, George Mkuchika wanasema hisia kwamba Chadema itashinda inatokana na tathmini ambayo imekuwa ikifanyika kutokana na taarifa za baadhi ya vyombo vya habari. “Vipo vyombo vya habari ambavyo vimedhamiria kuibomoa CCM. Wana CCM wafahamu kwamba vipo vyombo vitasema wana CCM wanaiba kura. Wanabusanda wategemee ushindi mkubwa,” alisema Mkuchika hivi karibuni. Katika kuonyesha namna ambavyo CCM kimeweka msingi katika ngazi ya kijiji jimboni Busanda, Mkuchika alisema walikuwa na timu sita za kampeni zilizohakikisha kwamba zinazungukia vijiji vyote 70 vya jimbo hilo.
Categories: