Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Kashfa ya Richmond kuibuka tena bunge lijalo

-
Rehema Mwinyi.

PAMOJA na macho na masikio ya Watanzania kuelekezwa bungeni kwa ajili ya bajeti ya serikali mapema mwezi ujao, kashfa ya Richmond iliyotikisa nchi mwaka jana itaibuka tena, safari hii serikali ikieleza ilipofikia katika utekelezaji wa maazimio 23 ya bunge.

Bunge lililotoa maazimio hayo na kuitaka serikali kuyatekeleza, lakini zoezi hilo limekuwa likisuasua na mara kwa mara kuibua maswali, hasa katika eneo la kuwawajibisha vigogo na watumishi wa umma waliotajwa na Kamati ya Dk Harrison Mwakyembe iliyochunguza kashfa hiyo kuwa walihusika kwa namna fulani katika kashfa hiyo.

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, alisema jana kuwa katika mkutano wa 16 wa bunge utakaoanza Juni 9, mwaka huu pamoja na taarifa hiyo ya Richmond, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo atatangaza bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010.

Taarifa hiyo ya Richmond imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu, kutokana na umuhimu wake kwa jamii, hasa baada ya kuwahusisha vigogo wa serikali na kusababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wengine wawili kujiuzulu.

Dk Kashililah alizitaja taarifa nyingine zitakazotolewa na serikali ni juu ya utendaji usioridhisha wa Kampuni ya Kupakua Makontena Bandarini (TICTS) pamoja na kuyumba kwa uendeshaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), uuzwaji wa nyumba za serikali pamoja na utoaji wa vitalu vya kuwindia.

Dk Kashililah hakufafanua kwa undani kuhusu kauli hizo za serikali, lakini kumbukumbu za gazeti hili zinaonyesha kuwa suala la Richmond linatokana na maazimio 23 ya Mkutano wa 10 wa Bunge uliofanyika Februari mwaka jana.

Miongoni mwa maazinio hayo, serikali ilitangaza kwenye mkutano wa 14 wa bunge kuwa inaendelea kuyachunguza, likiwamo la uchunguzi wa tuhuma dhidi ya vigogo na watumishi wa umma ambao walitajwa kuhusika kwenye kashfa hiyo.

Vigogo wanaoendelea kuchunguzwa kuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah.

Serikali pia inatarajia kutoa kauli juu ya uchunguzi maalumu uliofanywa ili kubaini ukweli kama taarifa halisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu Richmond iliharibiwa ili kutoa nyingine inayowasafisha vigogo dhidi ya ufisadi.

Vile vile serikali inatarajiwa kutoa jibu juu ya madai kwamba jalada halisi la kampuni ya Richmond lililokuwa kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) nalo liliharibiwa na kuwekwa jingine kwa lengo la kuficha ukweli.

Kumekuwepo na hali ya ukosoaji juu ya serikali kuwaruhusu baadhi ya vigogo wanaotuhumiwa kwenye kashfa hiyo ya Richmond kuendelea na nyadhifa zao wakati kuna uchunguzi dhidi yao.

Hali hiyo pia ilijidhihirisha kwenye mkutano wa 14 wa Bunge, ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, William Shellukindo akisoma taarifa ya kamati, alisema hali hiyo inatia shaka.

“Kamati ina maoni kwamba uwajibishwaji wa watumishi hao upewe kipaumbele kwa kuwa wao binafsi na nafasi ambazo bado wanazishika huku wakiendelea kuchunguzwa zinatia shaka juu ya utendaji wao wakati huu wa kuchunguzwa,” alisema Shellukindo.

Bunge lilitoa maazimio 23 ya utekelezaji baada ya mjadala wa taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa Novemba 2007 ili kuchunguza mchakato wa zabuni ulioipa ushindi Richmond ili kuzalisha umeme wa dharura nchini mwaka 2006.

Ripoti hiyo ya Kamati Teule ya Bunge juu ya Richmond ilisababisha pamoja na Lowassa kujiuzulu kwa mawaziri Dk Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi waliowahi kuwa mawaziri wa Nishati na Madini kwa nyakati tofauti.

Katika hatua za utekelezaji wa maazimio hayo, Agosti mwaka jana serikali ilivunja mkataba na Richmond ambao ulikuwa umerithiwa na kampuni ya Dowans.

Kuhusu kampuni ya TRL, Waziri wa Miundombinu, Dk Shukuru Kawamba anatarajia kutoa taarifa kuhusu kamati ya majadiliano iliyoundwa ili kurekebisha mkataba wa ukodishwaji baina ya serikali na Shirika la Reli la India (Rites).

Kumekuwepo na hali ya kutoridhishwa juu ya uendeshaji wa kampuni ya TRL ambapo baadhi ya shughuli zimesimamishwa na kumekuwepo na msuguano wa mara kwa mara juu ya maslahi ya wafanyakazi.

Kuhusu kampuni ya Ticts, Dk Kawambwa alikuwa ameliahidi bunge kuwa wizara yake itawasilisha mbele ya Baraza la Mawaziri waraka ambao utaainisha marekebisho ya mkataba wa kampuni hiyo na serikali, ili kupitishwa.

Awali, mkataba baina ya serikali na Ticts ulionekana kuwa na mapungufu kadhaa yakiwepo ya kutoruhusiwa kuwa na mshindani jambo ambalo liliibana serikali kuongeza nguvu baada ya uwezo wa kampuni hiyo kupungua na kusababisha msururu mrefu wa meli zinazosubiri kupakuliwa.

Hali hiyo licha ya kuwakatisha tamaa watumiaji wa bandari ya Dar es Salaam, iliisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha kwa kuwa kila meli iliyocheleweshwa kupakuliwa ilikuwa inalipwa Sh20 milioni kila siku.

Wakati huo huo, Dk Kashililah alisema kuwa kuanzia kesho kamati mbalimbali za bunge zitaanza kufanya vikao vyake vya kujadili kuhusu mambo mbalimbali ya bajeti.

Leave a Reply