Maafisa wa safari za ndege wa Ufaransa wamesema vifaa vya kunakili safari ya ndege iliyotoweka katika bahari ya Atlantic huenda visipatikane.
Maafisa hao walisema watafanya uchunguzi kwa makini mno, lakini walisema kazi yao wanaitekeleza katika mazingira ya hali ngumu mno.
Ndege hiyo, nambari AF 447, ilitoweka siku ya Jumatatu ilipokuwa safarini kutoka Rio nchini Brazil, ikielekea Paris, nchini Ufaransa, na ikiwa na abiria 228.
Mabaki ya ndege hiyo yameonekana kilomita 650 (maili 400) kutoka pwani ya Brazil, na wanamaji wa nchi hiyo wamekuwa wakifanya uchunguzi zaidi katika eneo hilo.
Maafisa wa Brazil na Ufaransa wamesema hakuna shaka mabaki yaliyopatikana ni ya ndege iliyotoweka.
Baadhi ya vitu vya kwanza kabisa kuonekana ni mafuta yaliyomwagika, kiti cha abiria na vinginevyo.