Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuunda Tume kuchunguza chanzo cha kuzama kwa meli ya MV Fatih ikiwa na abiria na mizigo katika Bandari ya Malindi ya Zanzibar.
Meli hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuja Zanzibar ilizama Ijumaa iliyopita baada ya kukumbwa na tatizo la kuingiza maji ikiwa katika mkondo wa bahari, hatua iliyosababisha mabaharia kutumia mashine kumwaga maji.
Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, aliiambia Nipashe kwamba tume hiyo itaangalia sura nzima ya tukio, hasa ubora wa chombo hicho pamoja na kupitia ripoti mbali mbali za ukaguzi wa meli hiyo.
Alisema iwapo kutabainika kwamba kuna uzembe ulikuwepo, hatua zitachukuliwa kwa wahusika kulingana na sheria.
Alisema kumejitokeza matapeli wanaodai wao ni waathirika wa ajali hiyo tangu serikali ilipotangaza itawasaidia watu walioaathirika.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Vuai Iddi Lila, alisema idadi ya abiria bado inaleta utata kwa vile watu waliosalimika idadi yao sasa imefikia 33 na waliokufa ni sita. Orodha ya awali ilidai kuwa abiria walikuwa 25 na mabaharia 13.
Wakati huo huo Kazi ya kuiopoa meli hiyo katika bandari ya Malindi iliendelea jana lakini hadi alasiri chombo hicho kilikuwa bado hakijaopolewa.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirika la Bandari, Abdi Omar, alisema chombo cha kunyanyua vitu vizito maarufu kama ndovu, kiliharibika ghafla katika sehemu ya jenereta na kukwamisha zoezi hilo. Alisema mafundi walikuwa wanaendelea kutengeneza.
Awali Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Generali Davis Mwamnaynge na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Said Mwema walitembelea eneo la tukio na kuwataka askari wa uokozi kuzidisha ushirikiano ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.