Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Kiti cha ndege chakutwa kikielea

-
Rehema Mwinyi.

Kiti, koti okozi, vipande vya chuma na dalili za mafuta vimeonwa katikati ya Bahari ya Atlantic na rubani wa Jeshi la Brazil ambaye ni mmoja wa wataalamu wanaoitafuta ndege ya Shirika la Ndege la Ufaransa, Air France, iliyopotea tangu juzi. Mabaki hayo yalionekana jana kutoka angani umbali wa kilometa 650 Kaskazini mwa kisiwa cha Brazil cha Fernando de Noronha, karibu na njia ambayo ndege hiyo ilipitia kabla ya kupotea ikiwa na watu 228, msemaji wa Jeshi la Anga, Jorge Amaral alisema jana. Licha ya kuonekana mabaki hayo, bado hakukuwa na dalili zozote za uhai katika maeneo mawili tofauti yaliyokutwa na mabaki hayo yaliyoachana umbali wa kilometa 60.

"Maeneo yalikopatikana mabaki hayo ni kuelekea pale ambapo ishara ya mwisho kutoka ndege hiyo ilipoonekana kwa waongoza ndege na kisha ikashindwa kuonekana tena," Amaral alisema. "Hiyo inamaanisha kuwa ilijaribu kukata kona, pengine ikitaka irudi Fernando de Noronha, lakini hizo ni hisia tu." Amaral alisema Serikali isingeweza kuthibitisha kuwa mabaki hayo yanatokana na ndege hiyo hadi hapo itakapokuwa imeopolewa kutoka ndani ya maji na kuitambua. Meli za kivita za Brazil zinatarajiwa kufika eneo la tukio leo.

Ugunduzi huu umekuja muda wa zaidi ya saa 24 baada ya ndege hiyo kuripotiwa kutoweka na kusababisha hofu ya watu wote waliokuwamo kupoteza maisha. Waokoaji bado wanaendelea na msako katika eneo pana la bahari hiyo kuanzia Kaskazini Mashariki mwa Brazil hadi pwani ya Afrika Magharibi. Ndege hiyo aina ya Airbus A330 yenye umri wa miaka minne, ilipoteza mawasiliano Jumapili saa 4.14 usiku. Ujumbe uliotoka katika ndege hiyo muda mfupi kabla ya kutoweka, ulisema ilikuwa imepoteza msukumo wa hewa na kukabiliwa na matatizo ya umeme.

Leave a Reply