Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Mwanajeshi aliyeshambulia polisi afungwa miaka 12

-
Rehema Mwinyi.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Bukoba imemhukumu askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Koplo Katarama, kifungo cha miaka 12 jela, baada ya kupatikana na hatia ya makosa matatu likiwamo la kumchania sare za kazi askari Polisi wa kike, kuharibu simu ya upepo na kumchania nguo ya ndani.

Hukumu hiyo ilitolewa Januari 5 mwaka huu katika Mahakama hiyo na Hakimu Richard Maganga ikielezwa kuwa mtuhumiwa ambaye hakuwa mahakamani hapo siku hiyo, alitenda makosa hayo Desemba 7, 2007 saa mbili asubuhi, eneo la Rwamishenye mjini hapa wakati polisi huyo akiwa kazini.

Awali Mahakama hiyo ilielezwa na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Ibrahimu Jumanne, kuwa Koplo Katarama siku hiyo alisimamishwa Rwamishenye akiwa katika gari la kiraia na wanajeshi wengine na baada ya gari kusimama, aliteremka na kumshambulia Sajini Wigesa aliyesimamisha gari hilo.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alimkaba polisi huyo na kumwangusha katika barabara ya lami na kumsababishia michubuko magotini na maumivu makali kichwani, huku akimchania mavazi yake, kuharibu simu, kofia ya Polisi na kumchania nguo ya ndani.

Jumanne alidai kuwa mshtakiwa alimzuia polisi huyo kufanya kazi yake na baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha mashahidi watatu, mtuhumiwa alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo hicho.

Katika kosa la kwanza la kumzuia polisi kufanya kazi yake na la kumjeruhi askari huyo, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano huku kwa la kumchania nguo, kuharibu simu na kofia alihukumiwa miaka miwili.

Leave a Reply