Wananchi wamelazimika kuvunja nyumba ili kumuokoa Muhsin Ali Said alipoamua kujifungia ndani jana mchana baada ya nyumba yake kuungua kwa moto.
“Aliamua kujifungia ndani akisema kwamba ni heri afe na nyumba yake. Vijana walilazimika kuvunja mlango na kumtoa kabla moto haujafika chumbani kwake na kumkimbiza msikitini. Ilikuwa ni hatari,” mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Abdul ambaye ni mmoja wa wanafamilia hiyo alisema jana katika eneo la tukio.
Abdul aliiambia Nipashe kwamba kwa takriban miezi kidhaa, Saidi alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya kiharusi na hivyo wakati nyumba yake iliyoko Mtaa wa Yombo, Temeke, Dar es Salaam inashika moto alikuwa ndani huku mkewe akiwa njiani akirejea kutoka safarini Morogoro.
Akizungumza kuhusu moto huo ulioteketeza kabisa nyumba hiyo, Abdul alisema kwamba ulitokana na pasi ya umeme.
“Kuna mfanyakazi wa ndani alikuwa akinyoosha nguo… Akajisahau kuzima pasi na ndio ikawa chanzo cha tukio hili,” alisema na kuongeza kwamba hakuna mtu aliyedhurika na moto huo.
Kwa mujibu wa Abdul, vitu vilivyookolewa na majirani baada ya kuvunja eneo ambalo moto ulikuwa haujasambaa ni friji, sofa na jiko la gesi.
Majirani walikilalamikia kikosi cha zima moto kwa kuchelewa kufika katika eneo la tukio mapema licha ya kutaarifiwa mara tu baada ya nyumba hiyo kushika moto..
Walidai kwamba licha ya nyumba hiyo kuanza kushika moto saa sita na nusu mchana, kikosi cha zima moto kilifika eneo la tukio saa nane mchana (masaa mawili na nusu baadaye) na kukuta nyumba hiyo ikiwa imeshatetea kabisa kwa moto.
Categories: