Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Zanzibar yakubwa na uhaba wa petroli

-
Rehema Mwinyi.

Zanzibar inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta ya petroli hali inayotishia kuathiri sekta za uchumi.

Uhaba huo wa petroli umekuja huku Zanzibar ikiendelea kukabiliwa na ukosefu wa umeme kwa siku 42 mfululizo.

Uhaba wa mafuta umeanza kujitokeza wiki iliyopita na kusababisha baadhi ya wananchi wanaomiliki magari kulazimika kuyafungia majumbani na kuanza kutumia usafiri wa daladala na wengine kutembea kwa miguu.

Magari yanayotoa huduma hivi sasa ya usafiri ni yale yanayotumia mafuta ya dizeli lakini idadi kubwa ya magari yanayotumia petroli yamelazimika kusitisha huduma za usafiri na kusababisha msongamano wa watu katika vituo.

Kufuatia kuadimika kwa mafuta ya petroli, kumeibuka biashara ya magendo ambapo lita moja ya petroli imekuwa ikiuzwa kwa Sh. 2,000 badala ya 1,480.

Uchunguzi wa Nipashe umegundua kuwa mafuta ya petroli yamekuwa yakiuzwa kwa bei za ulanguzi nje ya vituo vya mafuta, hasa katika maeneo ya Kijangwani, Mikunguni Gulioni.

Kampuni zinazaoingiza mafuta Zanzibar ni Zanzibar Petrolium, GAPCO, pamoja na Kampuni ya United Petroleum, lakini wateja wake wamekuwa wakifika katika vituo na kuondoka bila ya kupata huduma hiyo.

Mafuta ya petroli yamechukua nafasi kubwa katika shughuli za kiuchumi baada ya Zanzibar kukosa huduma ya umeme kuanzia Desemba, mwaka jana, baada ya kifaa aina ya spliter kulipuka katika kituo cha Fumba.

Kiongozi mmoja mwandamizi kutoka Kampuni ya United Petroleum, alisema uhaba huo wa mafuta umejitokeza baada ya nishati hiyo kuadimika katika bandari ya Mombasa, Kenya kufuatia nishati hiyo kuchelewa kuwasili kutoka nje ya nchi.

Alisema uhaba huo wa mafuta katika bandari ya Mombasa, unatarajia kumalizika kuanzia Januari 30, mwaka huu kwa vile meli zenye mafuta zinatarajiwa kuwasili katika bandari hiyo.

Hata hivyo, alisema baada ya kujitokeza upungufu huo wa mafuta, waliamua kutafuta mafuta kutoka katika meli moja iliyofunga gati, katika Bandari ya Dar es Salaam, lakini hawakufanikiwa kutokana na meli hiyo kuwa katika foleni kubwa ya kusubiri kuteremsha mafuta Tanzania Bara.

Leave a Reply