Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

NECTA lawamani kwa kushusha ufaulu wa wanafunzi

-
Rehema Mwinyi.


WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe ameeleza sababu kubwa iliyosababisha kushuka kwa ufaulu wa elimu ya msingi katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka jana kuwa ni pamoja na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), kudhibiti uvujaji wa mitihani na uchache wa walimu uliopo nchini.

Profesa Maghembe alitaja sababu nyingine iliyosababisha wanafunzi kufanya vibaya katika mtihani wa darasa la saba mwaka jana kuwa ni kutokuwepo uwiano sawa wa matumizi ya vitabu katika shule za msingi kote nchini.

Akifungua mkutano wa siku tatu wa wadau wa elimu nchini mjini hapa juzi, Profesa Maghembe alisema kitendo cha Baraza la Mitihani la Taifa kudhibiti uvujaji wa mitihani, umesababisha kushuka kwa ufaulu kutokana na wanafunzi wengi kutegemea kupewa mitihani.

Alisema licha ya NECTA kudhibiti hali hiyo, bado wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakichukua mitihani iliyopita na kuichapa upya na baadaye kuiuza mitaani kwa madai kuwa hiyo ndiyo mitihani yenyewe.

Kutokana na hali hiyo, Profesa Maghembe alisema imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kwa wanafunzi kufanya vibaya kwa kuwa wamekuwa wakitarajia kuwa mitihani waliyonunua ndiyo watakayoifanya.

Profesa Maghembe alisema hakuna utaratibu wa shule zote nchini kuwa na kitabu kimoja kinachotumika katika kufundishia na badala yake kila shule imekuwa ikinunua kitabu ambacho inaona ni kizuri na kinafaa kufundishia.

Alisema kitendo cha biashara kuingia katika shule za msingi, kimechangia kuharibu elimu ya Tanzania ambapo aliwataka maofisa elimu wa mikoa na wilaya, maofisa elimu taaluma na taasisi za elimu kuangalia na kukubaliana kuchagua vitabu vinavyowiana ambavyo vitatumika kufundishia katika shule zote nchini.

Kutokana na wanafunzi kufanya vibaya katika mtihani wa darasa la saba mwaka jana, wadau wa elimu wakiwemo maofisa elimu wa mikoa na wilaya, maofisa taaluma wa mikoa na wilaya, wakuu wa vyuo vya ualimu na wakurugenzi wa halmashauri, wanakutana mjini hapa chini ya uenyekiti wa Waziri Maghembe kujadili kwa kina sababu nyingine zilizosababisha wanafunzi kufanya vibaya katika mtihani huo.

 

Leave a Reply