Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Michael Jackson: Mazishi yake dili



Mazishi ya Mfalme wa Pop Duniani Michael Jackson yamegeuka kuwa 'dili' la aina yake baada ya watu kibao kugombea nafasi ya kuhudhuria shughuli hiyo.

Taarifa zinaeleza kuwa hadi sasa, zaidi ya watu 500,000 wamejisajili kwa ajili ya kucheza bahati nasibu ya kuwania tiketi kiduchu, zinazotajwa kuwa ni 17,500 pekee ili kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Michael Jackson.

Uwanja wa mpira wa kikapu wa Staples Center Jijini Los Angeles ndio utakaotumika Jumanne ijayo kwa shughuli za kumuaga mwanamuziki huyo aliyefariki ghafla Alhamisi iliyopita.

Hata hivyo, wakati watu kibao wakiwania kushiriki mazishi ya mfalme huyo wa pop duniani, familia yake bado haijaeleza ni siku gani hasa atazikwa.

[ Read More ]

Aliyedaiwa kufa aibuka msibani,

KIJANA Frank Mboma (19) aliyedaiwa kufa katika mji wa Mbalizi kwa kupigwa na wananchi wenye hasira na kuzikwa eneo hilo juzi alizua tafrani baada ya kuibuka msibani akitokea Tunduma.

Sakataka hilo lilitokea Jumatano wiki hii katika kijiji cha DDC mji mdogo wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya Vijijini baada ya kijana huyo kufika nyumbani kwao na kukuta watu wameweka tanga.

Kitendo hicho kilizua tafrani na waombolezaji hao kutimua mbio wakidhani muzimu umeibuka.

Majira baada ya kusikia taarifa hizo, lilifuatilia hadi kijijini hapo, umbali wa kilomita 15 kutoka Mbeya mjini kujionea kulikoni.

Akithibitisha kutokea tukio hilo Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bw. Joines Mwalusanya, alisema kifo hicho kilitokea June 27 mwaka.

Alisema walipelekewa taarifa ofisi ya kijiji kuwa kuna kijana amepigwa na wananchi wenye hasira na amefia Hospitali ya Rufaa Mbeya.

Alisema waliambatana na ndugu wa kijana huyo kwenda kutambua maiti Hospitali ya Rufaa Mbeya na kubaini kuwa marehemu huyo alikuwa ni Frank.

Hata hivyo, alisema babu wa kijana huyo Mzee Joyasi Mboma alikataa kuwa kijana huyo si mjukuu wake Frank kutokana na kuonesha tofauti za sehemu fulani mwilini japo alionekana kufanana naye kwa sehemu kubwa.


Baadaye alisema bibi wa kijana huyo na kinyozi aliyekuwa amemnyoa, walithibitisha kuwa ndiye na kuamua kuchukua kibali Polisi na kuzika Juni 29 jioni na kuendelea na matanga nyumbani kwa Mzee Mboma eneo hilo la DDC.

Naye Mzee Mboma ambaye amemlea kijana huyo akitoa maelezo yake kwa waandishi wa habari alisema mjukuu wake aliondoka wiki moja kwenda Tunduma kutafuta maisha hadi aliposikia habari kwamba kuna maiti inayofanana naye na baada ya utata alikubali kuzika mwili huo.


Alisema kuwa alishangaa Jumatano kufuatwa na watu na kuambiwa mjukuu wake amefika eneo jirani na kwake na anaogopa kuingia ndani baada ya kuambiwa alikuwa amekufa na kuzikwa na watu wamekusanyika kwa ajili ya msiba wake.


"Nilikwenda ingawa ilikuwa usiku wa manane, nilishangaa kumkuta Frank akiwa hai. Nilimchukua na kuingia naye ndani, baada
ya kumhoji tuligundua kuwa ni mjukuu wangu na tuliyemzika siye,"alisema Mzee Mboma.

Alisema kuwa kesho yake walikwenda Polisi kutoa taarifa na kuambia waende na Frank kwa ajili ya mahojiano zaidi ili kuondoa utata.

Akiwa Polisi Frank alieleza kuwa baada ya kwenda Tunduma kutafuta maisha alijisikia roho ikiuma na kuamua kurudi kwao mara moja ndipo alipokuta msiba wake bandia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Bw.Advocate Nyombi hakupatikana kuzungumzia sakata hilo lakini ofisa mmoja katika ofisi yake ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa kuwa si msemaji, alisema wamepata taarifa za tukio hilo na walikuwa wanasubiri maelezo kamili kutoka kwa maafisa wa Jeshi hilo waliokuwa wakifuatilia tukio hilo.
[ Read More ]

AMUUWA MDOGO WAKE KWA KUMCHOMA KISU.

SIMON JOHN [29] mkazi wa Jaluo anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumuua mdogo wake kwa kumchoma na kisu huko Arusha.
Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Basilio Matei amesema kuwa mtuhumiwa alikamatwa baada ya kutokea kifo hicho na kukutwa na kisu kikiwa kimetapakaa damu.

Kamanda Matei alisema kuwa mtuhumiwa alimuuwa mdogo wake aliyetambulika kwa jina la George wakati wakiwa katika ugomvi wa kifamilia kati yao.

Amasema mtuhumiwa katika ugomvi huo alichukua kisu na kumchoma nacho sehemu za kifua na kumsababishia kifo hicho.

Hata hivyo Kamanda Matei alisema kuwa hadi anatoa taarifa hizi chanzo cha kutokea kwa ugomvi huo hadi mtuhumiwa huyo kuchukua uamuzi wa kumchoma na kisu ndugu yake huyo kilikuwa bado hakijajulikana.

Amesema mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi wa tukio hilo kukamilika.

source;nifahamishe.com
[ Read More ]

KAZI NGUMU KUZUIA HOMA YA NGURUWE


Zaidi ya nchi 100 duniani, miongoni mwao Kenya na Uganda, zinakabiliana na shambulio la homa ya nguruwe na sasa Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Dr Margaret Chan aonya kwamba itakuwa vigumu kujaribu kudhibiti ugonjwa huo..

Alikuwa akihutubia mkutano wa maafisa wa afya ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa mjini Cancun, nchini Mexico.

Dr Chan alisema hatua ya kufanyika kwa mkutano huo nchini Mexico ambako homa hiyo ilianzia, ni ishara kubwa ya kuwa na imani katika nchi hiyo.

“Mexico ni salama, inavutia na ni pahali penye ukarimu mkubwa.”

Alisema kwamba aina ya ugonjwa huo ya H1N1 si hatari mno kwa kuwa ni rahisi kwa mgonjwa kupata nafuu bila ya matatizo.

“Na hapo ndipo tunakumbana na changamoto; kuwapa watu nasaha ya kuelewa wakati wa kupata huduma za matibabu na wakati wa kutokuwa na hofu,” alisema Dr Chan.

Kenya imeripoti visa tisa vya watu ambao wana virusi hivyo. Wote ni wageni kutoka Uingereza ambako inakisiwa maambukizo yatakuwa mengi.

Uganda nayo pia imetangaza kisa kimoja cha ugonjwa huo.

Viongozi na wataalamu kutoka nchi 50 wanakutana mjini Cancun kwa siku mbili ili kujadili mikakati ya kudhibiti kusambaa kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa huo.

Tangu ugonjwa huo kuzuka karibu miezi miwili iliyopita, zaidi ya watu elfu 70 wameambukizwa na zaidi ya mia tatu kufariki dunia.

[ Read More ]

Aliyemzushia Mumewe Amembaka Atupwa Jela

Mwanamke mmoja wa nchini Uingereza ambaye alimshtaki mumewe akidai mumewe amembaka ili aweze kuvunja uhusiano wao na kisha ajirushe na mwanaume mwingine amehukumiwa kwenda jela miezi minne.
Michaela Lodge, alifanya mapenzi na mumewe Martin katika nyumba waliyokuwa wakikaa pamoja mwezi novemba mwaka jana halafu baadae aliwapigia simu polisi akidai mumewe amemshambulia na amembaka.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, polisi walimhoji mwanamke huyo kwa masaa 62 wakati mumewe alitupwa selo kwa masaa 12 na baadae kuachiwa kwa dhamana baada ya kusisitiza kuwa alifanya mapenzi na mkewe kwa hiari yake bila kumlazimisha.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 45 na mkazi wa mji wa Essex alitengeneza barua ya ushahidi miezi miwili baadae akisisitiza kuwa amebakwa na mumewe lakini hataki mumewe ashtakiwe.

Mwezi februari mwaka huu mwanamke huyo alimwandikia barua mumewe akikiri kuwa aliongopa madai ya kubaka.

"Siwezi kuendelea na kesi hii tena, wakati tulipopanda kitandani sote tulikuwa na hamu ya kufanya mapenzi, niliwaongopea polisi kuwa umenibaka" ilisema barua hiyo.

Bwana Lodge aliwaonyesha polisi barua hiyo ya mkewe na haukupita muda polisi walimkamata mkewe.

Akitoa hukumu, jaji Rodger Hayward Smith alisema "Yalikuwa ni madai ya kutisha uliyokuwa umeyapangilia mapema ili kumtoa maishani mwako".

Michaela, mama wa watoto watatu alihukumiwa jana kwenda jela miezi minne pamoja na maombi ya mumewe kuwa asamehewe adhabu ya kifungo jela.

source:nifahamishe.com
[ Read More ]

MTOTO PEKEE ALIYEOKOKA KATIKA AJALI YA NDEGE YA YEMENIA


Mtoto aliyenusurika kimiujiza kwenye ajali ya ndege ya Yemen Airways iliyodondoka kwenye bahari ya Hindi karibu na visiwa vya Komoro na kuua watu 152 ameelezea jinsi alivyonusurika kimiujiza kwenye ajali hiyo. Bahia Bakari mwenye umri wa miaka 14 ndiye abiria pekee aliyenusurika kwenye ajali ya ndege ya Yemenia, Airbus A310 iliyotokea alfajiri ya jumanne wiki hii.

Bahia aling'ang'ania mabaki ya ndege na kuelea juu yake kwa masaa 12 katika hali ya hewa mbaya na bahari ambayo imejaa papa wengi kabla ya waokoaji kufika na kumuopoa.

Mtoto huyo ambaye hali yake inaendelea vizuri baada ya kupewa matibabu nchini Komoro amerudi kwao Ufaransa kuungana na baba yake.

Kassim Bakari, baba wa msichana huyo, akiongea na vyombo vya habari vya Ufaransa alisema kuwa nilipoongea naye kwa simu aliniambia "Tuliona ndege ikiangukia kwenye maji, nilijikuta kwenye maji, niliwasikia watu wakiongea lakini sikuweza kumuona hata mtu mmoja. Nilikuwa kwenye kiza sikuona chochote".

"Baba sikuweza kuogelea vizuri, niling'ang'ania juu ya kitu, sijui ni kitu gani" alisema Bahia akimwambia baba yake.

Bakari ambaye ana watoto wengine watatu alisema kuwa aliposikia habari za ajali ya ndege hiyo, moja kwa moja alifikiria kuwa hatamwona tena mkewe na mtoto wake wa kwanza.

"Ni msichana mwenye aibu sana, sikufikiria kama angenusurika namna hii, Siwezi kusema hii ni miujiza bali ni matakwa ya mwenyezimungu" alisema Bakari.

Bakari alisema kuwa Bahia hadi sasa hajaambiwa kuwa mama yake amefariki.

"Walimwambia kuwa mama yako yupo chumba cha jirani ili kutomshtua lakini ukweli ni kwamba mama yake amefariki na sijui nani ataweza kumwambia" alisema baba wa mtoto huyo.

Waokoaji walimuokoa Bahia kwenye bahari ya Hindi kilomita 16 toka kwenye pwani ya Visiwa vya Komoro.

Waokoaji hao walisema kuwa Bahia alikuwa dhaifu sana wakati anaokolewa, hakuweza hata kulishika boya alilorushiwa na hivyo kumfanya mzamiaji kupiga mbizi na kumpandisha kwenye boti ambako alifunikwa na blanket na kupewa maji ya moto yenye sukari anywe wakati anawahishwa hospitali.

Watu wengi wamestaajabu jinsi mtoto huyo alivyonusurika ajali hiyo na kuelea kwa jumla ya masaa 12 kwenye bahari ambayo imejaa papa wengi tena akiwa hana hata life jacket.


source:nifahamishe.com
[ Read More ]

Mwanamuziki Diana Ross kupewa watoto Michael Jakson

Mwanamuziki mashuhuri wa Marekani, Diana Ross ametajwa katika wosia wa Michael Jackson kama mlezi wa watoto watatu wa Michael inapotokea mama yake Michael Jackson mwenye miaka 80 atakaposhindwa kuwaangalia.

Hayo yapo katoka Wosia wa Michael Jackson ulioandikwa mwaka 2002 ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu, ambapo ulitolewa jana katika mahakama kuu ya Los Angeles, katika wosia huo Michael Jackson hakumtaja mke wake wa zamani Debbie Rowe kuchukua nafasi yoyote ya kuwalea watoto hao.

Katika wosia huo Michael Jackson amesema ndoa yake na Debbie Rowe iliishavunjika na kiuhakika hali hiyo inamzuia Debbie kupata chochote kutoka kwa Michael Jackson.

Michael Jackson ameacha mali yenye thamani ya jumla ya dola za kimarekani zaidi ya milioni 500 kwa familia yake.

Michael Jackson amemtaja mama yake kuwa msimamizi mkuu na mlezi wa watoto wake watatu.

Wosia huo ulipelekwa mahakamani na mwanasheria wa zamani wa Michael Jackson aitwaye John Blanca na kiongozi wa wanamuziki wa zamani John Mclain ambao walikuwa marafiki wa Michael kibiashara, wote wawili katika wosia wa Michael wametajwa kuwa wasimamizi wa mirathi.

Hata hivyo, wosia huo umeshindwa kutoa mwongozo wa masuala kadhaa likiwemo la maziko ya Michael Jackson kwamba atazikwa vipi na wapi au kuhusu utajiri wake utagawanywa vipi.

Vyombo vya habari mbalimbali vilikuwa vikidai leo mwili wa marehemu Michael utaagwa na mazishi yatafanyika siku ya Jumapili taarifa ambazo familia ya marehemu imezikanusha, lakini hawajasema lini nguli huyo wa muziki atazikwa.

Diana Ross mwenye miaka 65 ambaye alikuwa rafiki wa Michael Jackson amesema ," Moyo wangu unauma sana kusikia kifo cha Michael, hivi sasa nipo katika sara kuwaombea watoto wa Michael na familia ya Jackson."

Mwanasheria wa Michael alisema alichelewa kupeleka wosia huo mahakamani kwa sababu alitaka familia ya Jackson kuupitia kwanza.

"Suala la msingi katika wosia huo ni kwamba Michael amemwandika mama yake kuwa msimamizi mkuu wa watoto wake kisheria,"alisema mwanasheria huyo aitwaye Blanca.

Wakati huo huo mtengeneza muziki mkongwe Quincy Jones amesema anaweza asihudhurie mazishi ya Michael Jackson.

Jones ambaye alimtengenezea Michael albamu tatu ambazo ni Thriller, Off the Wall na Bad, bado yupo katika huzuni kubwa kutokana na kifo hicho cha ghafla cha rafiki yake Michael Jackson.

Serikali ya Marekani imeingia katika zoezi la uchunguzi wa kifo cha Michael Jackson ambapo itawachunguza madaktari waliohusika na Michael, jinsi wanavyofanya kazi na vyanzo vyao vya kupata madawa.

[ Read More ]

KIBAKA AHARIBIWA SURA KATIKA NYUMBA YA BONDIA.


Gregory McCalium kabla na baada ya kupewa kichapo na babu ambaye ni bondia mstaafu

Kibaka aliyezamia kwenye nyumba ya babu mmoja nchini Uingereza mwenye umri wa miaka 72 na kuanza kumtishia kwa kisu bila kujua kwamba babu huyo alikuwa ni bondia mstaafu, aliambulia kipigo kilichoichakaza sura yake.
Kibaka huyo Gregory McCalium mwenye umri wa miaka 24 mkazi wa wa Oxford nchini Uingereza, alivamia kwenye nyumba ya jirani yake ambayo babu huyo alikuwa akiishi na mke na kujaribu kuwapora mali zao bila kujua kwamba babu huyo alikuwa bondia mstaafu.

Babu Frank Corti mwenye umri wa miaka 72 alikuwa ni bondia maarufu enzi za ujana wake akiwa amejikusanyia vikombe kadhaa katika mashindano mbali mbali ya ndondi nchini Uingereza.

Picha iliyotolewa na polisi wa Uingereza ilionyesha jinsi sura ya kibaka huyo aliyekuwa na kisu ilivyoharibiwa vibaya na ngumi nzito za babu huyo.

Babu Corti baada ya kumwangushia kipondo McCalium alimlaza chini na kumlalia mpaka polisi walioitwa na mkewe walipokuja kumchukua.

Jumanne wiki hii McCalium alihukumiwa kwenda jela miaka minne na nusu kwa kosa hilo la jinai.

"Mwanzo nilishtuka aliporusha kisu chake, lakini kama watu wengine jinsi ambavyo wangejihami na mimi niliamua kufanya hivyo" alisema Corti.

"Umepata ulichostahili" alisema mwendesha mashtaka Angela Morris akimwambia McCalium wakati akisomewa mashtaka yake mahakamani hapo.

Tukio hilo lililotokea mida ya asubuhi lilimwacha kibaka McCallium akiwa amepasuliwa chini ya jicho lake na amechanika mdomo wake.

source:nifahamishe.com
[ Read More ]

SIMU ZA MKONONI ZAANZA KUSAJILIWA TZ.



ZOEZI la kusajili simu za mkononi kwa wananchi linaanza leo rasmi ili kudhibiti wimbi la wizi la bidhaa hizo nchini.
Zoezi hilo liliazimiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania [|TCRA] ili kuondoa kero zote zinazohusiana na zinazotokana na simu hizo za mkononi nchini.

Akitoa tamko hilo rasmi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, John Nkoma amesema kuwa zoezi hilo litaanza leo Julai Mosi, la kusajili kadi za simu za mkononi kwa wananchi.

Amesema kuwa lengo la kusajili kadi hizo ni kudhibiti matumizi mabaya ya simu yanayofanywa na wananchi vilevile ikiwemo na kupunguza wimbi la simu hizo ili kulinda maslahi ya mtumiaji.

Amesema ili kudhibiti matumizi mabaya ya simu sasa kila mwenye simu ya mkononi lazima ajiandikishe.

Amesema kila mwenye simu ya mkononi ni lazima ajiandikishe kwa kutumia vitambulisho maalumu vya kupigia kura, Passport ya kusafiria, kitambulisho cha mfuko wa pensheni, leseni za udereva.

Pia kwa wenye vitambulisho vya Saccos, Benki, ajira, kitambulisho cha chuo cha elimu ya juu, barua ya mwajiri na kama hivyo vyote hana unatakiwa uwe na barua ya serikali za mitaaa.

Amesema zoezi hilo linatarajiwa kufanyika kwa kipindi cha miezi sita na lengo la kusajili kadi hizo wananchi watakuja kutambua faida yake kwa wale ambao wanaona ni haisaidii.

Amesema kuwa wananchi wamekuwa wakitukanana kwa maneno mabovu kwa kununua namba na kuitupa pia kupeana maneno ya kutishana na kumekuwa kumeshamiri sana wizi wa simu hizo.

Amesema namba ya kadi ikishasajiliwa basi hata kama mtu akiiba simu hiyo hataweza kuitumia na matokeo yake ataitupa.
[ Read More ]

Mtoto wa miaka 14 ndio Abiria Pekee Aliyenusurika Ajali ya Yemen Airways



Mtoto wa miaka 14 ndiyo mtu pekee aliyenusurika kwenye ajali ya ndege ya Yemen Airways (Yemenia) ambayo ilidondoka jana kwenye bahari ya hindi ikiwa na jumla ya watu 153.
Waokoaji walisema kwamba msichana mwenye umri wa miaka 14 alikutwa akielea kwenye bahari ya Hindi kilomita 16 kutoka kwenye pwani ya visiwa vya Komoro.

Taarifa zilisema kwamba binti huyo aliyejulikana kwa jina lake la kwanza Bahia alikuwa akisafiri pamoja na mama yake.

Hali ya mtoto huyo inaendelea vizuri kwenye hospitali aliyolazwa kwenye visiwa hivyo.

"Anaendelea vizuri na aliweza kuongea na mamlaka husika na kuwaelezea kilichotokea" alisema msemaji wa timu ya waokoaji.

Taarifa za awali zilisema kwamba msichana huyo alikuwa na umri wa miaka mitano lakini msemaji huyo alikanusha taarifa hizo.

Ndege ya Yemen Airways (Yemenia) ilidondoka na kuzama kwenye bahari ya Hindi jana karibu na visiwa vya Komoro wakati ikitokea Ufaransa kuelekea Moroni, mji mkuu wa Komoro kwa kupitia Yemen ikiwa na abiria 153.

Watu wengi waliofariki ni raia wa Ufaransa na Umoja wa Ulaya ulisema ulikuwa na mpango wa kuzipiga marufuku kwenye anga ya ulaya ndege za Yemenia ambazo zimekosolewa sana kwa kuvunja taratibu za usalama.

Hii ni ajali ya pili ya ndege ambayo imepoteza maisha ya raia wengi wa Ufaransa ikiwa ni wiki chache baada ya ndege ya Ufaransa, Air France iliyokuwa ikitokea Brazili kuelekea Ufaransa ikiwa na abiria 228 kudondoka kwenye bahari ya Atlantic na kuua watu wote waliokuwemo kwenye ndege hiyo.

Yemenia kutokana na baadhi ya ndege zake kupigwa marufuku nchini Ufaransa ilikuwa ikitumia ndege zake mpya kwaajili ya nchi za ulaya na ndege zake za zamani kwaajili ya safari zake katika nchi za Afrika na kwingineko ambako hawakupewa masharti ya usalama wa ndege zao.

Ndege iliyotoka Ufaransa ilikuwa ni mojawapo ya ndege mpya za Yemenia na ndege hiyo ilipofika Yemen, abiria walibadilisha ndege na kupandishwa ndege hiyo ya zamani iliyokuwa inakuja Afrika ambayo ilipigwa marufuku nchini Ufaransa kutokana na matatizo yake mbali mbali.


[ Read More ]