Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Dereva wa teksi ashikiliwa kwa gari kutumika katika ujambazi

-
Rehema Mwinyi.

Polisi mkoani Singida inamshikilia dereva teksi kwa kosa la gari lake kuhusika na uporaji wa fedha Sh milioni nne mali ya mfanyabiashara wa alizeti, na baadaye kuvamia baa ya Kairo mjini hapa, na kutoweka na mauzo ya siku nzima.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Celina Kaluba matukio hayo yalitokea Jumanne na Jumatano wiki iliyopita katika eneo la Kibaoni na Mitunduruni katika Manispaa ya Singida.

Alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Said Juma (28) mkazi wa Majengo mjini hapa ambaye ni dereva anayeendesha teksi yenye namba za usajili 749 ABU na ubavuni ikiwa na namba 241. Alisema dereva huyo akiwa na wenzake ambao wanaendelea kutafutwa, wakiwa na silaha mbalimbali walifika nyumbani kwa mfanyabiashara Ruben Mhai (30) na kupora kwa nguvu Sh milioni nne zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye mkoba.

Kamanda huyo wa polisi alisema kabla ya kufanikisha unyang'anyi huo, Pendaeli Salumu (40) alijeruhiwa vibaya kwa kukatwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake, huku mlinzi wa nyumba Rajabu Salumu (38) akivunjwa mkono wa kushoto.

Alisema baada ya uhalifu huo, wezi hao wakiwa na gari hilo hilo, Jumatano walivamia tena baa ya Kairo iliyopo Mtaa wa Mitunduruni na kupora mauzo ya siku nzima ambayo hata hivyo kiasi chake hakijafahamika hadi sasa.

Alisema watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote upelelezi utakapokamilika. Katika tukio la tatu, Kaluba alisema wanamsaka dereva teksi Richard Ngoi baada ya kutoweka na gari hilo lenye namba za usajili T777 AAE Toyota mali ya Mary Mashuda (60) mkazi wa Mtaa wa Kibaoni.

Dereva huyo anadaiwa kutoweka na gari hilo Jumanne iliyopita wakati tajiri yake akiwa ndani ya Benki ya NMB kupatiwa huduma za kifedha, na alipotoka hakumwona tena mfanyakazi wake.

Kutokana na tukio hilo, Kaluba alisema wanamshikilia fundi magari wa gereji maarufu mjini hapa 'Vijana Garage,' Peter Mlay (25) kwa madai ya kushiriki wizi huo wa gari, na upelelezi unaendelea.

Leave a Reply