Watu wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama za kutaka kuiba zaidi ya Sh bilioni 6 mali ya Benki ya Stanbic. Akisoma mashitaka jana mbele ya Hakimu Nyigumalila Mwaseba, Mwendesha Mashitaka, Epifras Njau, alidai kuwa washitakiwa hao walikula njama za udanganyifu ili kutaka kuiba kiasi hicho cha fedha, jambo ambalo ni kinyume na sheria ya nchi.
Watuhumiwa hao walitajwa kuwa ni Kunji Meena (29), mfanyabiashara na mkazi wa Kurasini na Tumsifu Kimaro(33), dereva na mkazi wa Kurasini Shimo la Udongo, Dar es Salaam. Njau alidai kuwa, kati ya Mei 16 na 17 mwaka huu, watuhumiwa hao pamoja na wenzao ambao hawajafikishwa mahakamani, walikula njama za wizi Stanbic tawi la Sukari House. Aidha, alidai kuwa Meena anakabiliwa pia na tuhuma zingine mbili za wizi wa Sh 800,000 mali ya Tumsifu Kimaro ambaye ni mtuhumiwa wa pili katika kesi ya kwanza.
Njau alidai mbele ya Mwaseba kuwa kati ya Mei 16 na 17 mwaka huu, mtuhumiwa akitumia kadi ya ATM namba 0140518196401 alichukua Sh 400,000 siku ya kwanza na kiasi hicho hicho siku ya pili katika tawi hilo. Washitakiwa wote walikana mashitaka yao na wako nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana zilizowataka kuwa na wadhamini wawili ambao ni wafanyakazi wa Serikali au taasisi zinazotambulika na ahadi ya Sh 500,000 kila mmoja, kesi hiyo inatarajiwa kutajwa mahakamani hapo Juni 8 mwaka huu.
Categories: