Wizara ya Fedha na Uchumi Zanzibar imewatuhumu wahasibu wa kigeni wanaofanya kazi nchini kwa kushirikiana na wawekezaji kukwepa kulipa kodi na hivyo kuikosesha serikali mapato.
Akizungumza katika ufunguzi wa semina kwa jumuiya ya wahasibu na wakaguzi wa hesabu iliyofanyika jana mjini hapa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi, Abdi Khamisi Faki alisema zipo dalili zinazoashiria kuwa wahasibu hao hushirikiana na waajiri wao kufanya udanganyifu katika suala la kulipa kodi katika sekta mbalimbali ikiwamo hoteli za kitalii.
Alisema kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukwepaji wa kodi kwa baadhi ya wawekezaji wakishirikiana na wahasibu wa kigeni wanaowaajiri, serikali imekuwa ikikosa mapato, jambo linaloiathiri nchi kiuchumi na kusababisha hasara kubwa kwa taifa.
“Tuna idadi kubwa ya wahasibu kutoka nchi jirani wanaokuja kutafuta ajira na tuna mashaka kuwa wanashirikiana na wawekezaji wanaowaajiri kudanganya kulipa kodi,” alisema Faki huku akisisitiza kuwa serikali inafanya jitihada kukomesha suala hilo.
Alisema serikali inatafakari hatua za kuchukua juu ya suala hilo ikiwamo kuangalia uwezekano wa kuzuia ajira kwa wahasibu wa kigeni katika sekta hizo na badala yake ajira hiyo ifanywe na wazalendo tu.
Alisema kuwapo kwa wafanyakazi wazalendo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua tatizo hilo kwa kuwa itakuwa rahisi kwao kuweka maslahi ya taifa mbele na pia kutaongeza ajira kwa vijana wa Zanzibar na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.
“Hivi sasa serikali inaangalia uamuzi wa kuchukua juu ya tatizo hili, ikiwemo kuzuia ajira kwa wahasibu wa kigeni kwa kuwa ndio chanzo kikuu cha kukithiri kwa vitendo vya ukwepaji wa kodi nchini,” alisema.
Semina hiyo iliyowashirikisha wahasibu kutoka taasisi mbalimbali iliandaliwa na jumuiya ya wahasibu na wakaguzi Zanzibar kwa lengo la kuwaongezea uwezo wafanyakazi wa taaluma hiyo na kuwakumbusha wajibu wao.
Categories: