Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wameiomba Serikali kuimarishia ulinzi katika eneo la mahakama hiyo na wao binafsi. Maombi hayo yalitolewa jana na watumishi hao, mbele ya Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, alipotembelea mahakama hiyo. Akizungumza kwa niaba ya watumishi hao, Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Addy Lyamuya, aliiomba serikali kupitia kwa Chikawe, kuwaimarishia ulinzi watumishi wa mahakama hasa ikizingatiwa uzito wa kesi zinazosikilizwa hapo. Lyamuya alisema watumishi hao wanahitaji ulinzi huo wanapokuwa kazini na hata nyumbani, ili kudhibiti jambo lolote la hatari litakalowakumba.
Aliongeza kuwa, Jeshi la Polisi linatakiwa kuboreshwa, ili lifanye kazi ndani na nje ya mahakama huku changamoto kubwa ikiwa ni ya kukosa vitendea kazi vitakavyowasaidia kuimarisha ulinzi. Lyamuya alimwambia Chikawe kuwa mbali na matatizo hayo, mahakama ina mazingira duni ambayo ndiyo yanayotegemewa kusikilizia kesi hizo. Akisoma taarifa ya maendeleo ya mchakato wa utenganishaji wa shughuli za mashtaka na upelelezi katika mahakama hiyo, Msaidizi wa Mkurugenzi wa Mashtaka, Winfrida Kasoro, alisema mchakato umeleta mafanikio mengi ikiwa ni pamoja na uharakishwaji wa kesi mahakamani hapo.
Aliongeza kuwa mbali na mafanikio hayo, mchakato huo umepata changamoto nyingi kama kutopatikana mashahidi kwa wakati na mawakili kuacha kazi kutokana na kipato kidogo. Akijibu hoja zilizowasilishwa katika kikao hicho, Chikawe alisema atawasilisha matatizo hayo katika ngazi husika na pia aliishauri mahakama kuandika barua ya maombi ya kukarabatiwa kwa jengo hilo. Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuajiri wanasheria wapya, ili kukabiliana na utandawazi ikiwa ni pamoja na kuongeza kipato cha wafanyakazi wa mahakama.
Categories: