Zaidi ya asilimia 50 ya wanawake wajawazito mkoani Singida hujifungulia majumbani na kwa wakunga wa jadi, hali inayohatarisha usalama wa maisha yao na watoto wanaozaliwa. Hayo yalibainishwa na daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi Mkoa wa Singida, Dk. Christopher Mgonde kwenye mafunzo ya kuokoa maisha ya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Dk. Mgonde alisema ingawa takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya vifo vya wanawake wakati wa kujifungua mkoani Singida imepungua kutoka 61 mwaka juzi hadi 49 mwaka jana, lakini bado kuna tatizo kubwa la wajawazito wengi kutojifungulia kwenye vituo vya tiba.
Alisema miongoni mwa mambo yanayosababisha hali hiyo ni umbali mrefu kwenda kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali, mila na desturi na matusi kutoka kwa baadhi ya watoa huduma.
Alisema pamoja na mambo mengine ikiwamo elimu duni na matatizo ya kiuchumi, hizo ndizo sababu kuu zinazosababisha wengi wa wanawake kuhudhuria vizuri kliniki wakati wa ujauzito wao na kujifungulia majumbani badala ya vituo vya tiba. Dk. Mgonde alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, Idara ya Afya kupitia vitengo vyake mbalimbali inaendelea kutoa elimu kwa akinamama juu ya umuhimu wa kujifungulia kwenye vituo vya tiba.
Alisema lengo la hatua hiyo ni kupunguza kiwango cha vifo vya wajawazito na watoto wakati wa kujifungua ili kulinda kizazi na ustawi wa jamii kwa ujumla. Mafunzo hayo ya wiki mbili kwa watoa huduma za uzazi yameandaliwa na kuratibiwa kwa pamoja na Idara ya Afya Mkoa wa Singida na Taasisi ya Benjamin William Mkapa.
Categories: