Mahakama Kuu ya Tanzania inatarajia kuanza kusikiliza kesi tano za mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ‘albino’ katika miji ya Wilaya za Kahama na Shinyanga mkoani Shinyanga kuanzia Jumatatu. Kwa mujibu wa Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu, John Utamwa, kesi tatu zitasikilizwa mjini Kahama na Jaji Gabriel Rwakibarila kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na zimepangwa kusikilizwa kwa muda wa siku 35.
Utamwa alisema Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Kanda ya Dodoma, Gadi Mjemas anatarajiwa kusikiliza kesi nyingine mbili katika Mahakama Kuu mjini Shinyanga zilizopangwa kusikilizwa kwa muda wa siku 21. “Taratibu zote kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hizo zimekamilika,” alisema Utamwa.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Msemaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, Omega Ngole alisema tayari Mawakili wa Serikali wameshawasili katika miji ya Kahama na Shinyanga kwa ajili ya kuendesha kesi hizo ambazo upelelezi wake umekamilika. Kuanza kusikilizwa kwa kesi hizo, kunaifanya Tanzania kuungana na nchi za Rwanda na Burundi ambazo zimeanza kusikiliza kesi za aina hiyo hivi karibuni.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwapo na malalamiko ya kuchelewa kusikilizwa kwa kesi za mauaji ya albino nchini. Pia Mbunge kutoka Canada ambaye ni albino aliishinikiza nchi yake kuinyima misaada Tanzania kwa kile alichodai tatizo la mauaji hayo kutomalizika nchini. Licha ya malalamiko hayo, tayari serikali ilishafanya kura za maoni nchi nzima kwa watu kuwataja wanaohusika na biashara ya viungo vya albino.
Categories: