Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Mabomu yadhibitiwa, 17 hoi kwa mshtuko

-
Rehema Mwinyi.


Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jana lililipua mabomu 11 yaliyokuwa katika kambi yake iliyopo Mbagala Kuu ambapo wakazi 17 wa Mbagala walikumbwa na mshtuko na baadhi yao akiwamo mjamzito wa miezi tisa, walizimia na kupelekwa hospitalini.

Awali mamia ya wakazi wa eneo hilo lililopo wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam, waliamua kuyahama maeneo yao pamoja na kuwapo taarifa kuwa watulie majumbani kwa kuwa mabomu hayo yangedhibitiwa na yasingekuwa na madhara.

Mabomu yaliyolipuliwa jana, yaliokotwa katika makazi ya watu baada ya kutokea ajali katika kambi hiyo Apili 29 mwaka huu, iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 20 na uharibifu wa mali zikiwamo nyumba na samani za wananchi. Askari wa JWTZ jana walilipua mabomu hayo kati ya saa nne na saa tano asubuhi na kusababisha vishindo vikubwa na moshi mzito angani.

Wakati yanalipuliwa, mamia ya wakazi wa Mbagala hawakuwapo kwenye makazi yao, nyumba zilikuwa zimefungwa, baadhi wakiwamo wanawake na watoto waliokuwa njiani kwenda mbali na kambi hiyo wakikimbia athari za mabomu.

Bomu la kwanza lililipuliwa saa nne na dakika nne asubuhi, la 11 lililipuliwa saa tano na dakika 15 asubuhi, na ilipofika saa sita na dakika 11, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Said Mkumbo alitangaza kuwa kazi ya kuyalipua imekwisha. Mkumbo alisema, kazi hiyo ilifanywa vizuri, na kwamba uongozi wa wilaya ulijiandaa kuwahudumia waathirika na kulinda makazi ya wananchi ili vibaka wasiibe.

“Tulijiandaa kwa maana kwamba tulichukua tahadhari…tulijiandaa kwa sababu tulijua dharura yoyote inaweza kutokea,” alisema Mkumbo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la kambi ya Chama cha Msalaba Mwekundu ya kuwadumia waathirika wa mabomu hayo.

Wakati yanalipuliwa, sehemu nyingi za biashara jirani na kambi ya JWTZ zilikuwa zimefungwa, kulikuwa na watu wachache katika barabara iliyo jirani na kambi hiyo, na kwa ujumla jana asubuhi Mbagala ilikuwa kwenye hali ya tahadhari.

Kazi hiyo ya kulipua ilipokuwa ikiendelea, waandishi wa habari waliongozwa na Skauti kwenda jirani na eneo lililotumika kuyalipua, wakati wanakaribia, bomu lililipuka, wote wakatimua mbio kunusuru maisha. “Yaani wee, tulikuwa tumefika kabisa, nimechanganyikiwa kabisa, yaani hata sijajua tumesambaratika vipi, naona tu vyuma taap, yaani hata sijui wameondoka vipi (waandishi wengine),” alisema Anne Robi wa gazeti la Daily News.

“Yaani mimi naona watu wanakimbia ikabidi na mimi nikimbie…nilikuwa nakimbia naona viatu vinanichelewesha, nikajiuliza nivue nini,” alisimulia Robi. “Nilihisi kila bomu likilipuka hereni yangu inafunguka kwa nini?” Aliuliza Kusiluka wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), mwenzake kutoka katika shirika hilo, Rachael Mhando alimjibu huku wakionekana kuogopa” eti eeh, let’s go my dear, stori tutapata huko.”

Mkazi wa Mtoni Kijichi, Juma Mdelele alidai kuwa, taarifa ya JWTZ kuhusu ulipuaji ilikuwa tofauti na hali halisi kwa sababu kama wananchi wangeifuata kauli hiyo na kuendelea na shughuli zao athari zingekuwa kubwa. Mdelele alidai kuwa, alikwenda katika Hospitali ya Temeke kumpeleka mmoja wanawake walioathiriwa na milipuko hiyo akakuta wengine 10 na akashauri kuwa JWTZ ingewaamuru wananchi wawe umbali fulani kutoka kambini hapo ili kuepusha madhara.

“Wangetoa tu tangazo jamani tutalipua, kaeni mbali, halafu waongeze tu ulinzi, lakini kuwambia watu waendelee na shughuli zao hapana,” alisema. Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano JWTZ Jumatano wiki hii iliwahakikishia wakazi wa Mbagala kuwa, milipuko ingekuwa salama kwa kuwa ingedhibitiwa lakini iliwataka wananchi wakae mbali na eneo la kulipulia.

Jana alasiri, Msemaji wa JWTZ, Alfred Mbowe alisema, kwa ujumla kazi ya kulipua mabomu ilifanywa vizuri na hakukuwa na madhara kwa askari na wananchi. Meneja Habari wa Red Cross, Stella Marialle alisema, inawezekana baadhi ya wananchi walibaki kwenye makazi yao kulinda mali zao na walizingatia pia taarifa ya JWTZ kuwa yasingekuwa na madhara.

“Majeruhi wameletwa na tumewapeleka Temeke hospitali, tathmini ya haraka hawapungui kumi, lakini taarifa kamili tutaipata Temeke hospitali,”alisema Marialle wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kambi ya kuhudumia waathirika wa mabomu. “Nafikiri mabomu ni mabomu, ikitokea wakati mwingine wananchi waondolewe hata kama ni kwa nguvu,” alishauri.

Akizungumza kwa niaba ya Mwakilishi wa Kamishna wa Skauti Wilaya ya Temeke, Rehema Marango, aliyewasimamia Skauti jana, Alphonce Mabula alisema, baadhi ya waathirika walikutwa katika makazi yao, na kwamba, wakazi wengi wa Mbagala waliondoka jana asubuhi kwenda mbalii na eneo la kambi ya Jeshi.

Wakati mabomu yakilipuliwa, magari ya Polisi yenye namba za usajili, PT 1524 na PT 1161 aina ya Land Rover 110 yalikuwa yakifanya doria, wafanyakazi 25 wa Chama cha Msalaba Mwekundu na Skauti 15 walikuwa wakiwahudumia waathirika wakiwamo waliopoteza fahamu.

Magari matatu ya Red Cross yenye namba za usajili, T 563 AMA, T 127 ARS na T590 AFM yalikwenda maeneo mbalimbali kuwachukua waathirika na kuwapeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke. Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Asha Mahita alisema, waathirika 17 wa mabomu hayo walifikishwa katika hospitali hiyo akiwamo mjamzito huyo, Mboni Chano (23) anayeishi Njia Panda ya Kijichi, wanawake wengine 14 na wanaume wawili.

Kabla ya kufikishwa hospitalini hapo, 'Habari Leo Jumapili' ilimwona mjamzito huyo akiwa hajitambui jirani na ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mbagala Kuu. Gazeti hili lilikuta waathirika hao wakiwamo wanawake 14, wakiwa katika hospitali hiyo, wengi wao walikuwa wamepata fahamu, Dk. Mahita alisema walikuwa wakiendelea vizuri.


Leave a Reply