Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Serikali ya Zanzibar yazuia waandishi kuingia bandarini

-
Rehema Mwinyi.

BAADA ya waandishi wa habari kupinga kunyanyaswa na askari wa vikosi vya serikali ya mapinduzi wakati wa ziara ya Rais Amani Abeid Karume juzi, Idara ya Habari ya serikali hiyo, jana ilizuia waandihi wa habari wa vyombo mbalimbali kuingia bandarini.

Miongoni mwa waandishi waliozuiwa ni wa vyombo vya habari binafsi pamoja na vya serikali ya Jamhuri ya Muungano, likiwepo Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Hatua hiyo ilidhihirika bada ya waandishi kadhaa kuzuiwa kuingia katika Bandari ya Zanzibar ambako kwa zaidi ya wiki sasa wamekuwa wakifika kufuatilia mwenendo wa harakati za uokoaji kutokana na ajali ya kupinduka kwa meli ya Mv Fatih.

Waandishi hao walipofika kwenye bandari hiyo walikuta orodha ya majina ya waandishi zaidi ya 10, ambao wamepigwa marufuku kuingia bandarini.

“Aah! Leo mmeumia, hamtaweza kuingia humu ndani kwa mujibu wa maelekezo tuliyopewa,” alisema mmoja wa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao walikuwa wakiongoza ulinzi bandarini hapo.

Askari huyo ambaye hakutaka kutaja jina alisema amepewa majina ya watu ambao wasingeruhusiwa kuingia bandarini humo jana.

“Sisi tunafanya kazi kwa maagizo. Amekuja Bosi wenu Juma (Afisa habari wa Maelezo Zanzibar) kasema wenye majina haya wasiingie labda muwasiliane naye,” alifafanua.

Waandishi waliozuiliwa ni wa magazeti, vituo binafsi vya televisheni na redio, lakini vyombo vinavyomilikiwa na SMZ waliruhusiwa ingawa nao waliungana na wenzao katika kugomea kufanya kazi wakati wa ziara ya Rais Karume.

Mkurugenzi wa Maelezo Zanzibar, Hassan Mitawi alisema hakuwa na taarifa zozote kuhusu kuzuiwa kwa waandishi hao, lakini akaahidi angefuatilia suala hilo.

Pia Mkurugenzi wa Shirika la Bandari la Zanzibar, Mustpha Aboud Jumbe alipopigiwa simu alisisitiza kuwa uongozi wa bandari haujatoa ilani yoyote ya kuwazuia waandishi wa habari na wala hawana taarifa juu ya kizuizi hicho.

Hata hivyo, juzi jioni baada ya askari hao kuwazuia waandishi katika ziara ya Rais Karume, alikuja Makamu wa Rais Ali Shein na kutembelea eneo hilo, lakini hali ilibadilika kwani waandishi waliachwa kuendelea na kazi na hata kufanya mahojiano naye.

Dk Shein alipongeza jitihada zilizofanywa na wataalamu wa Shirika la Bandari Zanzibar kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na vikosi mbalimbali vya majeshi.

Dk Shein alisema watu wawe na subira na wawape nafasi wataalamu wafanye kazi yao na baadaye itakapomalizika watapata taarifa.

Habari zilizopatikana jana jioni zilieleza kuwa operesheni hiyo imefungwa baada ya wazamiaji kuingia melini na kukuta hakuna maiti iliyosalia.

Kazi iliyofanyika ni kuondoa baadhi ya mali zilizokuwamo miongoni zikiwemo nondo na mbao.

Kwa sasa inasubiriwa Jumatatu ili kuiondoa meli hiyo katika eneo la bandari ili kuweza kuruhusu shughuli nyingine kuendelea kama kawaida.

Leave a Reply