Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

MABOMU ZAIDI LEO,MBAGALA WALILIA CHAKULA.

-
Rehema Mwinyi.



Wakati mchakato wa kukamilisha ripoti ya fidia kwa wananchi walioathirika kwa milipuko ya mabomu katika eneo la Mbagala, Dar es Salaam ikiendelea kufanyiwa kazi, baadhi ya wakazi hao jana ‘walivamia’ ofisi za kata wakidai kutopatiwa msaada wa chakula kama inavyostahili. Wakazi hao walikusanyika kwa wingi katika ofisi hizo, kuanzia majira ya saa 2:00 asubuhi huku miongoni mwao wakiwa wanawake waliokuwa wamebeba watoto. Aidha, wakati wamekusanyika, wengine walisikika wakisema sio wote wenye matatizo ingawaje hawawezi kufikia kiwango kikubwa kama ambavyo walikusanyika katika eneo hilo. Akizungumzia hali hiyo, Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, Anderson Chale aliwasihi wananchi hao kurudi katika makazi yao na kwamba kazi ya ugawaji chakula ingewafikia huko baada ya kuwasiliana na viongozi wao wa mitaa kwa kuwa baada ya kuzungumza na viongozi wenzake, wamebaini kuwa sio wote wenye madai hayo. Hata hivyo, tamko hilo la Diwani lilipingwa na wananchi hao waliopiga kelele za kukataa, wakidai kutokuwa na imani na viongozi hao badala yake kutakiwa kuchagua viongozi watakaowaamini miongoni mwao, jambo ambalo walilifurahia kwa pamoja na kukubaliana nalo. Diwani aliwatahadharisha kutoingiza majina ya ndugu zao katika suala hilo ili kwamba waonekane kuwa wako wananchi wengi wenye matatizo ya aina hiyo, na kwamba wazingatie taratibu za kupatiwa chakula kwa kuwa tayari zilishaelezwa tangu awali. Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Temeke, Said Mkumbo, alisema watakachofanya ni pamoja na kuangalia orodha ya majina waliyonayo ya wakazi wa kata hiyo na kazi ya kuwagawia chakula itafuata utaratibu huo maalumu. Alisema watendaji husika wanaendelea kufuatilia suala hilo kwa maana kuwa si kila mmoja akifika hapo adai chakula apewe bila kuzingatia taratibu zinazotakiwa. Naye mkazi wa Mwanamtoti, Abdallah Hafidh, alisema ni kweli wapo wenye matatizo ambao hawajapata kabisa chakula na wengine kidogo, lakini kwa waliokusanyika jana siyo wote wenye shida. Mkazi wa Mbagala Kuu, Neema Makofa, alisema tangu kazi ya ugawaji chakula ianze katika kata hiyo kwani hajapata chakula hivyo, alitoa mwito kwa uongozi huo kupatiwa huduma hiyo. Kuhusu ulipuaji wa mabomu leo, Mkuu wa Wilaya alisema ofisi yake ikishirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), wamejiandaa kwa kuweka tahadhari za kutosha huku baadhi ya wakazi wakisema wana taarifa na wengine wataondoka katika makazi hayo ili kupisha usumbufu unaoweza kujitokeza.



Leave a Reply