Mwanamke mmoja Jijini ameuawa kinyama kwa kuchinjwa na kisha kichwa chake na kiwiliwili kutengenishwa.
Inadaiwa mwanamke huyo ameuawa na mtu anayedaiwa kuwa ni mume wake.
Tukio hilo la mauaji ya kinyama, linadaiwa kutokea jana katika maeneo ya Kigogo Jijini.
Taarifa ambazo Alasiri imezipata, zinaeleza kuwa aliyetekeleza mauaji hayo ya kinyama ni mume wa mwanamke huyo ambaye alitoroka baada ya tukio.
Hata hivyo, majina ya marehemu na mtuhumiwa wa mauaji hayo hayakuweza kuthibitishwa.
Aidha, taarifa zaidi zimedai kuwa chanzo cha mauaji ya mwanamama huyo anayedaiwa kuacha watoto wawili ni wivu wa kimapenzi.
Hata hivyo, Mwandishi alipojaribu kumsaka Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mark Kalunguyeye, ili aelezee tukio hilo, hakuweza kupatikana kupitia simu yake ya mkononi.
Naye Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema hajapata taarifa za tukio hilo.
Aliposakwa tena Kalunguyeye, mtu aliyepokea simu alidai kuwa Kamanda Kalunguyeye alikuwa ameelekea katika hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale Mabibo ambako kulitarajiwa kufanyika mkutano wa Kamati ya Ulinzi ya Mkoa na Uongozi wa Chuo hicho.
Categories: