Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Padri akemea ngono UDSM

-
Rehema Mwinyi.

Padri Josephat Mosha wa Kanisa Katoliki Parokia ya Chang’ombe mkoani Dar es Salaam, amewataka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kutambua na kuzingatia kilichowapeleka chuoni hapo na kuachana kabisa na dhana potofu ya kudanganyana kuhusu uhusiano.

“Katika maisha haya ya shule, mara nyingi sana wengi wetu huwa tunapotoshana kuhusu neno upendo na kufikia mahali mtu anasahau hata kile kilichomleta mahali hapa kutokana na kuzama katika suala hilo, itakuwa vyema kama mtajiuliza kuwa mmefuata nini mahali hapa ili kuepuka kuhatarisha maisha yenu,” alisema Padri Mosha.

Padri Mosha alikuwa akizungumza kwenye Ibada ya kumuombea marehemu Beatha Mwarabu (23), aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) cha UDSM ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumapili kwa kuchomwa kisu na mwanafunzi mwenzake, Masaba Musiba anayedaiwa alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi kwa muda mrefu.

Alisema vijana wengi wa siku hizi wamekosa upendo kwa kile alichoeleza kuwa hali hiyo imetokana na vijana hao kutokuwa tayari kusikiliza maneno ya watu muhimu katika jamii, wakiwamo wazazi wao na hivyo kusababisha vijana hao kuwa na watu wenye chuki pamoja na visasi ambapo ili kuepukana na hayo yote, aliwataka kwanza kujifunza dhana itokanayo na neno upendo.

“Mtu hawezi kujipenda yeye kwanza kabla hajampenda mwenzake, hivyo mioyoni mwetu yatupasa kujenga tabia ya kuwapenda wenzetu kabla ya kujipenda sisi,” alisema Padri Mosha. Aidha, Padri Mosha aliwataka watu wote kutambua kwamba kila mmoja ataonja mauti hata kama ataishi miaka mingapi, na kuwaasa kutubu dhambi zao na kumcha Mungu.

Mapema, majonzi, simanzi na vilio vilisikika kwa wingi jana katika ukumbi uliopo katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Chang’ombe wilayani Temeke, wakati walimu, wanafunzi, ndugu na jamaa walipokuwa wakiuaga mwili wa mwanafunzi Beatha aliyefariki usiku wa kuamkia Jumapili baada ya kuchomwa kisu na Musiba aliyedaiwa kuwa ni mpenzi wake.

Hali ya huzuni chuoni hapo ilikuwa imetawala tangu tangu juzi baada ya kutolewa kwa taarifa na kubandikwa kwa matangazo yaliyoelezea tukio la kifo hicho pamoja na kilichosababisha, huku baadhi ya wanafunzi wakiwa bado wameshikwa na butwaa na kutoamini kile kilichotokea. “Inasikitisha sana yaani mpaka muda huu wengi wetu bado hatuamini kwamba kweli mwenzetu katutoka tena kwa kifo cha kinyama kiasi hiki, ila kwa upande wetu tutazidi kumuombea kwa Mungu huko aendako,” alisema mmoja wa wanafunzi wa DUCE, Mwanahamisi Shaabani.

Kwa upande wake, baba mdogo wa marehemu, Rafael Mwarabu alisema kifo hicho kimewasikitisha na zaidi wanamuomba Mungu amzidishie heri huko aendako na kueleza kuwa tangu kipindi cha uhai wake, Beatha alikuwa mtu mwenye tabia njema na heshima kwa kila mtu. Kwa upnde wake, Mkuu wa Elimu chuoni hapo, Joviter Katabalo alimwelezea Beatha kwamba alikuwa mwanafunzi mwenye bidii chuoni hapo kwa kujituma wakati wote pamoja na kushirikiana vizuri na wanafunzi wenzake hadi anakutwa na mauti.

Alisema kifo hicho kimekuwa pigo kubwa kwa upande wa wanachuo chuoni hapo. Mwili wa marehemu ulisafirishwa jana na unatarajiwa kuzikwa leo katika Kijiji cha Kibaoni kilichopo Ifakara katika Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. Kwa mujibu wa taarifa za wanafunzi wenzao, wakiwamo marafiki wa karibu wa marehemu, Beatha na mtuhumiwa walianza mapenzi muda mrefu tangu wakiwa wanafunzi wa shule mkoani Morogoro.

Inaelezwa kuwa tangu waanze masomo chuoni hapo, uhusiano wao haukuwa mzuri kutokana na ugomvi wa mara kwa mara huku chanzo kikubwa kikidaiwa ni tabia ya ulevi aliyokuwa nayo mvulana ambayo mwenzake alichukizwa nayo. Wote wako walikuwa mwaka wa pili DUCE.

Inadaiwa Beatha alimpa mpenziwe mwezi mmoja wa kujirekebisha kutokana na tabia hiyo na kumtishia kusitisha uhusiano wao endapo angeendelea na tabia hiyo, lakini pamoja na hilo mpenzi wake huyo hakujirekebisha na ndipo msichana akachukua uamuzi wa kusitisha uhusiano huo; hatua ambayo bila ya shaka ndiyo iliyosababisha mvulana achukue hatua ya kumchoma kisu na kumuua.




Leave a Reply