Moto mkubwa umelipuka katika jengo la Golden Sand lililopo kwenye Mtaa wa Karume pale Oysterbay Jijini na kusababisha mali zenye thamani ya mamilioni ya fedha kuteketea.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mark Kalunguyeye, amesema moto huo ulianza jana mishale ya saa 1:00 asubuhi na kuunguza chumba kimoja cha jengo hilo, ambalo ni mali ya Bw. Fidar Hussein.
Amesema chumba namba tisa cha jengo hilo ambacho kinatumika kama jiko, ndicho kilichoteketea kwa moto uliounguza vitu tele vilivyokuwamo ndani.
Kamanda Kalunguyeye amesema miongoni mwa vitu vilivyoteketea kwa moto ni pamoja na jokofu moja kubwa lililokuwa ndani ya chumba hicho.
Akasema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme na kwamba thamani ya mali iliyoteketezwa na moto huo bado haijafahamika.
Kwa mujibu wa Kamanda Kalunguyeye, moto huo ulizimwa na Kikosi cha Zimamoto cha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo.
Categories: