Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Mahabusu wa Guantanamo awasili New York


Maafisa wa Marekani wameeleza mahabusu wa kwanza wa gereza la Guantanamo, atakayeshitakiwa katika mahakama ya kiraia ya Marekani amewasili New York.

Ahmed Ghailani amepelekwa kukabiliana na mashtaka katika mahakama ya New York akihusishwa na uripuaji wa mabomu wa balozi za Marekani katika Afrika Mashariki.

Bwana Ghailani, Mtanzania, alikamatwa nchini Pakistan mwaka 2004. Anatazamiwa kufikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama ya Manhattan baadae siku ya Jumanne.

Alipelekwa Guantanamo akiwa pamoja na mahabusu wengine wanaoitwa "muhimu sana" mwishoni mwa mwaka 2006.

Kuhamishwa kwake kumekuja huku Rais Obama akiwa katika hekaheka za kutafuta utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa wakati wa uchaguzi ya kufunga gereza la Guantanamo Bay katika kipindi cha mwaka mmoja akiwa madarakani.

Waandishi wa habari wanasema kesi ya Bwana Ghailani litakuwa jaribio muhimu katika mipango ya utawala wa Obama kufunga gereza hilo na hatimaye kuwafikisha mbele ya sheria watuhumiwa.

Serikali ya Marekani ina matumaini ya kuwasafirisha baadhi ya watuhumiwa wengine katika baadhi ya nchi, lakini hadi sasa mashauriano juu ya hilo yamekwama hasa iwapo Marekani nayo ipo tayari kupokea mahabusu.

Baraza la Congress lilikataa maombi ya serikali ya kugharamia kufungwa gereza la Gauantanamo, kukiwa na upinzani mkali wa kuwapeleka watuhumiwa Marekani.

[ Read More ]

Mahabusu Keko wagoma kula

KESI za mahabusu wa gereza la Keko, jijini Dar es Salaam, waliogoma kula kushinikiza kesi zao kusikilizwa, zitaanza kuunguruma Mahakama Kuu ya Tanzania, mwezi huu.

Habari za kuaminika ambazo gazeti hili imezipata kutoka kwa maofisa wa Gereza hilo mwishoni mwa wiki, zilieleza kuwa tayari kesi hizo zimewekwa kwenye kalenda ya mahakama.

Ufafanuzi huo ulitolewa na mmoja wa maofisa wa gereza hilo, aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la jina lake kutochapishwa gazetini, kufuatia kuwepo taarifa za mahabusu kuanza mgomo.

"Hapa hakuna mgomo wa mahabusu kwa sababu wote wameishaelezwa kuwa kesi zao zinasikilizwa mwezi huu," kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya gereza hilo.

Alisema ndani ya gereza hilo wapo mahabusu wanaotaka kuishinikiza Serikali iwe inafanya kila kitu wanachotaka,jambo ambalo halikubaliki.

Chanzo hicho kilifafanua kuwa ndani ya gereza hilo wapo wafungwa wanaoshinikiza migomo. "Mahabusu hao ni miongoni mwa wanaoanzisha migomo wakati wanajua wazi kuwa kesi zao zipo mbioni kuanza kusikilizwa," alisema.

Wiki iliyopita baadhi wa mahabusu katika gereza hilo walipenyeza ujumbe kwa njia ya simu kwenye vyombo vya habari juu ya kuwepo kwa mgomo wa kugomea chakula ili kushinikiza kesi zao zianze kusikilizwa.

Baadhi ya mahabusu hao, walidaiwa hali zao ni mbaya, madai ambayo yalikanushwa na mmoja wa maofisa wa gereza hilo.

Ofisa huyo alidai kuwa awali mgomo wa mahabusu hao ulikuwa ni wakutaka kesi zao zisikilizwe. "Kama tayari mahakama imewapangia tarehe ya kusikilizwa kwa kesi zao ni kitu gani wanataka?"alihoji ofisa huyo.

Mwaka jana mahabusu wa gereza hilo waligoma kula wakipinga kesi zao kutopangiwa tarehe za kusikilizwa.

Mahabusu hao walikuwa wakihoji sababu za kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Bw.Abdallah Zombe, na wenzake ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini kusikilizwa haraka wakati wao wamekaa muda mrefu gerezani bila kesi zao kupangiwa tarehe ya kusikilizwa.

Mgomo huo ulimlazimu maofisa waandamizi wa Idara ya Mahakama na Wizara ya Sheria na Katiba kuwatembelea gerezani na kuzungumza nao.
Mwisho
[ Read More ]

Mtoto aunguzwa Dar kisa chakula!

Hali ya afya ya mtoto Comfort Kimaro, 7 wa Mbezi Saranga Jijini Dar bado haijatengemaa na anaendelea kuuguzwa katika Hospitali ya Tumbi wilayani Kibaha kutokana na majeraha mabaya ya moto yaliyotokana na kile kinachodaiwa kuwa ni kuunguzwa moto na mke wa baba yake mdogo.

Taarifa zinadai kuwa mtoto huyo, aliunguzwa mwilini kwa mkasi wa moto na mke wa baba yake mdogo anayetajwa kwa jina la Domina Kimaro, kutokana na kosa la kula chakula kilichokuwa kimehifadhiwa kwa ajili ya msichana wa kazi almaarufu kama hausigeli.

Inaelezwa kuwa Comfort ameunguzwa kwa kutumia mkasi uliokuwa ukiwekwa kwenye mafuta ya moto na mke huyo wa baba yake mdogo (Domina) na kisha kupitishiwa mwilini mwake mara kadhaa kwa ni ya kumuadhibu.

Taarifa zinadai kuwa tukio hilo limejiri hivi karibuni, mishale ya saa 4:00 usiku baada ya kubainika kuwa mtoto huyo alikula chakula cha msichana wa kazi.

Imeelezwa kuwa siku ya tukio, mama huyo (Domina) alipandwa na hasira aliposikia kuwa Comfort amekula chakula cha msichana wa kazi na kuamua kuchukua hatua hiyo ya kumuunguza mwilini kwa mkasi uliokuwa ukichemshwa kwenye mafuta ya moto na kumbabua mwilini tena na tena.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mark Kalunguyeye, amesema polisi wanamshikilia mtuhumiwa Domina na kesho wanatarajia kumpandisha kizimbani.

Aidha, akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Habari wa Shirika la Elimu Kibaha, ambaye pia ni Afisa uhusiano wa Hospitali ya Tumbi Bw. Gerald Chami, amesema hali ya Comfort bado haijawa nzuri na hivyo anaendelea kulazwa ili apate matibabu zaidi.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa majirani ndio waliomfikisha mtoto huyo hospitalini baada ya kumtwaa toka kwa Bi. Domina aliyekuwa ameshamuunguza mwilini bila huruma na kumuacha ndani pasi na kumpeleka jospitalini.

Mjumbe mmojawapo wa eneo hilo la Mbezi Saranga, Bw. Christopher Francis, amesema kuwa siku ya tukio, mtoto huyo alikuwa akipiga kelele nyingi za kuomba msaada.

Akasema majirani walipojaribu kwenda kumsaidia, wakashindwa kwa vile Domina alikuwa ameufunga mlango wa nyumba na kuendelea kumuadhibu akiwa ndani.

Hata hivyo, akasema yeye na majirani wengine wakaenda tena siku nyingine na kufanikiwa kumpata mama aliyefanya ukatili huo ambaye kazi yake ni kupika na kuuza chakula katika eneo la Saranga Temboni.

Akasema baada ya kumpata walimuhoji kuhusina na adhabu hiyo, lakini mama huyo akakana kuwa hakumuunguza.

Akasema baada ya kuona mama huyo anakwepa tuhuma, walimua kumuhoji msichana wa kazi wa mama huyo ambaye ndiye aliyetakiwa kula chakula kile kinachodawa kuliwa na mtoto Comfort.

Mjumbe huyo wa shina akasema msichana huyo wa kazi ndiye aliyefichua kuwa mtoto huyo alichomwa na mama yake mdogo kwa kutumia mkasi uliokuwa ukilowekwa kwenye mafuta ya moto.

Bw. Fransis akasema kwa kushirikiana na wananchi, waliamua kutoa taarifa Polisi na mama huyo akapelekwa kituoni kwa ajili ya kutoa maelezo zaidi.

Akasema baadaye majirani waliamua kuchangishana fedha na kupata zaidi ya shilingi 60,000 walizozitumia kumpeleka mtoto Comfort katika hospitali ya Tumbi, ambako hadi sasa anaendelea kutibiwa.

Aidha, alipohojiwa, Comfort amesema mama yake mdogo alikuwa na tabia ya kumpiga mara kwa mara, hasa baba yake mdogo aitwaye Geofrey Kimaro anapokuwa safarini.

Akasema siku ya tukio baba yake mdogo alikua safarini na hakupewa chakula tangu asubuhi hadi jioni na ilipofika mishale ya saa 10:00 jioni, mama yake mdogo alimpa chakula ili akipeleke nyumbani kwa msichana wao wa kazi.

Akasema kwa vile yeye (mtoto) alikuwa na njaa kutokana na kuwa alikuwa hajala chochote, aliamua kukila na ndio maana akajikuta akiunguzwa moto kwa kosa hilo.

Akasema mama huyo alimuunguza kwa kutumia mkasi alioukuwa akiuloweka kwenye mafuta ya moto.

Hata hivyo, akasema baada ya kuunguzwa huko, mama yake mdogo (Domina) hakumpeleka hospitali na badala yake akawa anampaka yai, hali iliyomfanya awe akipata maumivu makali zaidi.

Kwa upande wa mama mzazi wa mtoto huyo Elinani Lalashowi, 36, mkazi wa Moshi ambaye alifika juzi kumuuguza mwanawe baada ya kupata taarifa kutoka kwa shemeji yake aitwae Vicent, amesema hana la kuongea kwa sasa kwani hakuwahi kuwa na ugomvi wowote na mke huyo wa shemeji yake.

[ Read More ]

mbunge wa busanda akaribishwa bungeni


Mbunge wa Busanda, Lolesia Bukwimba (mbele kulia), akisindikizwa na wabunge wanawake wa Chama Cha Mapinduzi kuingia bungeni ili kula kiapo jana baada kushinda uchaguzi mdogo wa jimbo hilo uliofanyika Mei 24, mwaka huu.
[ Read More ]

Basi laua watano Dodoma

WATU watano wamekufa baada ya basi la abiria kupinduka leo saa tano asubuhi wakati likitoka Dar es Salaam kwenda mkoani Singida.

Basi hilo liitwalo, Hajjiz, aina ya Scania lilipinduka baada ya tairi ya mbele kupasuka.

Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dodoma, Salum Msangi amesema, basi hilo lenye namba za usajili T 441 AYN lilipinduka saa 5.40 katika kijiji cha Mtumba, takribani kilomita 17 kutoka mjini Dodoma.

Inadaiwa kuwa watu wanne walikufa papo hapo, mwingine alifariki dunia wakati akikimbikizwa hospitali.

Kwa mujibu wa Msangi, walioshuhudia ajali hiyo wamedai kuwa basi hilo lilikuwa kwenye mwendo mkali, na baada ya ajali dereva alikimbia polisi wanamtafuta.
[ Read More ]

Umeme waua mume, mke taabani Muhimbili

Baba mmoja amefariki dunia na mkewe kujeruhiwa vibaya baada ya kuangukiwa na waya wa umeme.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Faustine Shilogile amemtaja marehemu kuwa ni Masari Abdulhussein, 27, na aliyejeruhiwa kuwa ni Bi. Najma Swalehe, 24, wote wakazi wa Kigamboni.

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Shilogile amesema watu hao wamekutwa na mkasa huo wakati wakiwa wamebebana kwenye pikipiki.

Amesema tukio hilo la kusikitisha limetokea katika eneo la makutano ya barabara za Uhuru na Nyamwezi, Kariakoo Jijini.

Akasema Bw. Masari ndiye aliyekuwa akiendesha pikipiki hiyo yenye namba za usajili T 311 AMS aina ya Sangly huku akiwa amembeba mkewe na kuwa walipofika eneo hilo, waliangukiwa na waya wa umeme wenye moto na kusababisha wajeruhiwe vibaya.

Kamanda Shilogile amesema wataalam wa Shirika la Umeme nchini, Tanesco waliitwa mara moja na walipofika wakawatoa na kuwakimbiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Akasema hata hivyo mwanaume, alifariki dunia wakiwa njiani na mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Taifa, Muhimbili.

Amesema mkewe Bi. Najma naye amelazwa hospitalini hapo ambapo anaendelea kupewa matibabu.
[ Read More ]

Moto wateketeza mali za mamilioni Oysterbay Dar

Moto mkubwa umelipuka katika jengo la Golden Sand lililopo kwenye Mtaa wa Karume pale Oysterbay Jijini na kusababisha mali zenye thamani ya mamilioni ya fedha kuteketea.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mark Kalunguyeye, amesema moto huo ulianza jana mishale ya saa 1:00 asubuhi na kuunguza chumba kimoja cha jengo hilo, ambalo ni mali ya Bw. Fidar Hussein.

Amesema chumba namba tisa cha jengo hilo ambacho kinatumika kama jiko, ndicho kilichoteketea kwa moto uliounguza vitu tele vilivyokuwamo ndani.

Kamanda Kalunguyeye amesema miongoni mwa vitu vilivyoteketea kwa moto ni pamoja na jokofu moja kubwa lililokuwa ndani ya chumba hicho.

Akasema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme na kwamba thamani ya mali iliyoteketezwa na moto huo bado haijafahamika.

Kwa mujibu wa Kamanda Kalunguyeye, moto huo ulizimwa na Kikosi cha Zimamoto cha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo.

[ Read More ]

Mama achinjwa Dar

Mwanamke mmoja Jijini ameuawa kinyama kwa kuchinjwa na kisha kichwa chake na kiwiliwili kutengenishwa.

Inadaiwa mwanamke huyo ameuawa na mtu anayedaiwa kuwa ni mume wake.

Tukio hilo la mauaji ya kinyama, linadaiwa kutokea jana katika maeneo ya Kigogo Jijini.

Taarifa ambazo Alasiri imezipata, zinaeleza kuwa aliyetekeleza mauaji hayo ya kinyama ni mume wa mwanamke huyo ambaye alitoroka baada ya tukio.

Hata hivyo, majina ya marehemu na mtuhumiwa wa mauaji hayo hayakuweza kuthibitishwa.

Aidha, taarifa zaidi zimedai kuwa chanzo cha mauaji ya mwanamama huyo anayedaiwa kuacha watoto wawili ni wivu wa kimapenzi.

Hata hivyo, Mwandishi alipojaribu kumsaka Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mark Kalunguyeye, ili aelezee tukio hilo, hakuweza kupatikana kupitia simu yake ya mkononi.

Naye Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema hajapata taarifa za tukio hilo.

Aliposakwa tena Kalunguyeye, mtu aliyepokea simu alidai kuwa Kamanda Kalunguyeye alikuwa ameelekea katika hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale Mabibo ambako kulitarajiwa kufanyika mkutano wa Kamati ya Ulinzi ya Mkoa na Uongozi wa Chuo hicho.

[ Read More ]

kwa heri Beatha.


Baadhi ya waombolezaji wakitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE), Beatha Mwarabu (picha ndogo) aliyeuawa kwa kuchomwa kisu na mwanafunzi mwenzake. Heshima za mwisho zilitolewa jana chuoni hapo Chang’ombe, Dar es Salaam.
[ Read More ]

Padri akemea ngono UDSM

Padri Josephat Mosha wa Kanisa Katoliki Parokia ya Chang’ombe mkoani Dar es Salaam, amewataka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kutambua na kuzingatia kilichowapeleka chuoni hapo na kuachana kabisa na dhana potofu ya kudanganyana kuhusu uhusiano.

“Katika maisha haya ya shule, mara nyingi sana wengi wetu huwa tunapotoshana kuhusu neno upendo na kufikia mahali mtu anasahau hata kile kilichomleta mahali hapa kutokana na kuzama katika suala hilo, itakuwa vyema kama mtajiuliza kuwa mmefuata nini mahali hapa ili kuepuka kuhatarisha maisha yenu,” alisema Padri Mosha.

Padri Mosha alikuwa akizungumza kwenye Ibada ya kumuombea marehemu Beatha Mwarabu (23), aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) cha UDSM ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumapili kwa kuchomwa kisu na mwanafunzi mwenzake, Masaba Musiba anayedaiwa alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi kwa muda mrefu.

Alisema vijana wengi wa siku hizi wamekosa upendo kwa kile alichoeleza kuwa hali hiyo imetokana na vijana hao kutokuwa tayari kusikiliza maneno ya watu muhimu katika jamii, wakiwamo wazazi wao na hivyo kusababisha vijana hao kuwa na watu wenye chuki pamoja na visasi ambapo ili kuepukana na hayo yote, aliwataka kwanza kujifunza dhana itokanayo na neno upendo.

“Mtu hawezi kujipenda yeye kwanza kabla hajampenda mwenzake, hivyo mioyoni mwetu yatupasa kujenga tabia ya kuwapenda wenzetu kabla ya kujipenda sisi,” alisema Padri Mosha. Aidha, Padri Mosha aliwataka watu wote kutambua kwamba kila mmoja ataonja mauti hata kama ataishi miaka mingapi, na kuwaasa kutubu dhambi zao na kumcha Mungu.

Mapema, majonzi, simanzi na vilio vilisikika kwa wingi jana katika ukumbi uliopo katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Chang’ombe wilayani Temeke, wakati walimu, wanafunzi, ndugu na jamaa walipokuwa wakiuaga mwili wa mwanafunzi Beatha aliyefariki usiku wa kuamkia Jumapili baada ya kuchomwa kisu na Musiba aliyedaiwa kuwa ni mpenzi wake.

Hali ya huzuni chuoni hapo ilikuwa imetawala tangu tangu juzi baada ya kutolewa kwa taarifa na kubandikwa kwa matangazo yaliyoelezea tukio la kifo hicho pamoja na kilichosababisha, huku baadhi ya wanafunzi wakiwa bado wameshikwa na butwaa na kutoamini kile kilichotokea. “Inasikitisha sana yaani mpaka muda huu wengi wetu bado hatuamini kwamba kweli mwenzetu katutoka tena kwa kifo cha kinyama kiasi hiki, ila kwa upande wetu tutazidi kumuombea kwa Mungu huko aendako,” alisema mmoja wa wanafunzi wa DUCE, Mwanahamisi Shaabani.

Kwa upande wake, baba mdogo wa marehemu, Rafael Mwarabu alisema kifo hicho kimewasikitisha na zaidi wanamuomba Mungu amzidishie heri huko aendako na kueleza kuwa tangu kipindi cha uhai wake, Beatha alikuwa mtu mwenye tabia njema na heshima kwa kila mtu. Kwa upnde wake, Mkuu wa Elimu chuoni hapo, Joviter Katabalo alimwelezea Beatha kwamba alikuwa mwanafunzi mwenye bidii chuoni hapo kwa kujituma wakati wote pamoja na kushirikiana vizuri na wanafunzi wenzake hadi anakutwa na mauti.

Alisema kifo hicho kimekuwa pigo kubwa kwa upande wa wanachuo chuoni hapo. Mwili wa marehemu ulisafirishwa jana na unatarajiwa kuzikwa leo katika Kijiji cha Kibaoni kilichopo Ifakara katika Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. Kwa mujibu wa taarifa za wanafunzi wenzao, wakiwamo marafiki wa karibu wa marehemu, Beatha na mtuhumiwa walianza mapenzi muda mrefu tangu wakiwa wanafunzi wa shule mkoani Morogoro.

Inaelezwa kuwa tangu waanze masomo chuoni hapo, uhusiano wao haukuwa mzuri kutokana na ugomvi wa mara kwa mara huku chanzo kikubwa kikidaiwa ni tabia ya ulevi aliyokuwa nayo mvulana ambayo mwenzake alichukizwa nayo. Wote wako walikuwa mwaka wa pili DUCE.

Inadaiwa Beatha alimpa mpenziwe mwezi mmoja wa kujirekebisha kutokana na tabia hiyo na kumtishia kusitisha uhusiano wao endapo angeendelea na tabia hiyo, lakini pamoja na hilo mpenzi wake huyo hakujirekebisha na ndipo msichana akachukua uamuzi wa kusitisha uhusiano huo; hatua ambayo bila ya shaka ndiyo iliyosababisha mvulana achukue hatua ya kumchoma kisu na kumuua.




[ Read More ]